KARAMA ZA ROHO
MTUMISHI WA MUNGU
SOMO: KARAMA ZA ROHO
MTUMISHI WA MUNGU
UTANGULIZI
Siku za Yesu hapa duniani zilitiwa uzito kwa miaka kama mitatu ya huduma ambayo llionekana kuwa kiini na kusudi la uhai wake. Mara zote Bwana wetu Yesu alionyesha upendo na huruma kwa kuwahudumia wale waliomzunguka ambao walikuwa na mizigo ya magonjwa, pepo, dhambi, udhaifu na mambo yafananayo na hayo. Hakuishia hapo bali alitoa ahadi kwa wote watakaomwamini kufanya yote alioyafanya na hata zaidi (YN 14:12).
Twaona baada ya kifo na ufufuko wa Yesu akiwaambia wanafunzi wake kungoja ahadi ya Baba huko Yerusalemu. Baadaye twaona ubatizo wa Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste kwa wanafunzi, nguvu hii iliambatana na dhana za ujenzi wa kanisa ulio mwili wa Kristo ambao ni karama za kiroho. Kwa hiyo, kiini cha karama ni Bwana wetu Yesu kristo atendaye kazi ndani yetu kupitia Roho wake (MDO 1:4-8; 2:1-4, GAL 2:20).
Mtume Paulo alipata ufunuo na neema ya kueleza kwa undani zaidi jambo hili, hasa kwa kanisa la korintho. Neno lililokuwa kama kiini cha mafundisho haya kwa mtume Paulo ni hili “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana utofauti wa huduma, na Bwana ni yeye yule. Tena pana utofauti wa kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote” (1KOR 12:4-6). Madhumuni ya Paulo ni kuonyesha kwamba ingawa kuna karama mbalimbali ndani ya kanisa, zote zinatokana na Roho mtakatifu; pia ingawa kuna huduma mbalmbali ndani ya kanisa, zote zinatokana na Bwana Yesu; na kwa kumaliza ni kwamba kazi zinaweza kutendeka kwa namna tofauti ndani ya kanisa lakini ni Mungu ndiye mtenda kazi kupitia watu wote (1KOR 3:9). Mkazo mkubwa hapa ni kuonyesha kwamba huduma na karama vinatokana na nafsi ya Mungu mwenyewe (Baba, mwana na Roho Mtakatifu) na kuonekana kwa macho ya mwili kupitia watumishi wake.
Lakini la kushangaza twaona shetani kutumia vitu hivi vilivyoletwa na Mungu kwa ajili ya ujenzi wa kanisa lake. Anatumia kwa lengo la kuaribu kanisa la Mungu pamoja na watumishi wake. Hii ni kazi ya ibilisi kuharibu asili ya Mungu ndani ya wanadamu na kuwajaribu watumishi wa Mungu kupitia vitu walivyopewa na Mungu kama Amana ili vigeuze maana yake na kuwa jaribu.
Kitabu hiki ni sehemu ya tatu ya kitabu kinachosema “Mtumishi wa Mungu katika utumishi wake”. Malengo makubwa ni kuonyesha faida ya huduma na karama mbele za Mungu na mbele za watu, kuonyesha njia ambazo shetani anatumia ili kujaribu watu wa Mungu kupitia karama ili kuwatenganisha na muumba wao, pia tutaonyesha njia zitakazotusaidia kumshinda shetani ili Mungu atimize kusudi lake hapa chini ya jua kupitia sisi.
ENDELEA NA USOMAJI WA KITABU
SOMA SURA YA KWANZA →