MATRIX:SURA YA TANO

SURA YA TANO

Kuvunja Matrix: Safari ya Kurudisha Uhuru wa Akili

Baada ya kuelewa jinsi Matrix inavyofanya kazi, swali muhimu linabaki moja: Je, inawezekana kutoka ndani yake? Jibu ni ndiyo. Lakini kutoka ndani ya Matrix hakutokei kwa kubadilisha simu, kufuta akaunti za mitandao ya kijamii au kukimbilia kuishi mbali na watu. Matrix si kifaa. Matrix ni mfumo wa tabia. Na mfumo wa tabia huvunjwa kwa kujenga mfumo mwingine wenye nguvu zaidi. Uhuru wa kweli hauanzi nje yako. Unaanzia ndani ya akili yako.

Hakuna mtu anayeweza kukufanya uwe huru ikiwa wewe mwenyewe hujaamua kuiongoza akili yako.

Hatua ya Kwanza: Rudisha Umiliki wa Muda Wako

Muda ndiyo mali pekee ambayo kila binadamu amepewa kwa kiwango sawa. Tofauti kati ya watu wengi si muda waliopewa, bali namna wanavyoutumia. Anza siku yako bila kushika simu kwa dakika thelathini hadi sitini. Tumia muda huo kusali, kutafakari, kufanya mazoezi, kuandika malengo au kusoma kitabu. Ukianza siku kwa notifications, tayari umeikabidhi akili yako kwa watu wengine. Ukianza siku kwa kusudi lako, wewe ndiye umeiongoza akili yako.

Hatua ya Pili: Jenga Nidhamu ya Dopamine

Ubongo unahitaji kujifunza tena kufurahia kazi zinazohitaji uvumilivu. Soma kitabu. Andika. Jifunze ujuzi mpya. Tembea bila simu. Kaa kimya. Fanya kazi ngumu. Mwanzoni utaona ni vigumu. Hiyo ni ishara kwamba ubongo wako ulikuwa umezoea zawadi za haraka. Kadiri unavyoendelea kufanya kazi zenye maana, ndivyo mfumo wa zamani unavyopoteza nguvu.

Kanuni ya 24/1 Kwa kila saa moja unayotumia kwenye mitandao ya kijamii, tumia angalau dakika ishirini na nne kujifunza kitu kitakachoongeza thamani kwenye maisha yako. Usiruhusu burudani izidi maendeleo.

Hatua ya Tatu: Soma Vitabu Vinavyokupinga

Matrix hukua pale unaposikia sauti moja kila siku. Ukuaji huanza unapokutana na mawazo yanayokulazimisha kufikiri upya. Soma waandishi ambao hukubaliani nao. Sikiliza watu wenye mtazamo tofauti. Hoji kila jambo kwa heshima. Usiwe mtu anayelinda maoni yake; kuwa mtu anayelinda ukweli. Mwanafalsafa Socrates aliamini kuwa maisha yasiyochunguzwa hayastahili kuishi. Kauli hiyo inaendelea kuwa muhimu hata katika dunia ya kidijitali.

Akili yenye nguvu haiogopi maswali. Ni akili dhaifu inayokimbia ukweli.

Hatua ya Nne: Tumia Teknolojia Kama Mtumishi

Teknolojia si adui. Tatizo huanza pale ambapo nafasi hubadilika. Simu inapaswa kuwa kifaa cha kukusaidia. Isiigeuke kuwa bwana anayekuamuru kila dakika. Zima notifications zisizo muhimu. Panga muda maalumu wa kuingia mitandaoni. Usilete simu mezani wakati wa chakula. Usilale nayo kitandani. Mabadiliko haya madogo yanaweza kurejesha mamia ya saa ndani ya mwaka mmoja.

Hatua ya Tano: Tengeneza Zaidi Kuliko Unavyotumia

Matrix inapenda watumiaji. Dunia inahitaji wazalishaji. Badala ya kutumia saa tatu kutazama video za watu wengine, tumia sehemu ya muda huo kuandika makala, kurekodi mafunzo, kuanzisha biashara, kujifunza programu mpya au kutengeneza bidhaa. Kila unapozalisha thamani, unaondoka hatua moja ndani ya Matrix. Kila unapokuwa mtumiaji tu, unaendelea kuipa nguvu.

Jiulize kila jioni:
  • Leo nimezalisha nini?
  • Nimejifunza nini?
  • Nimemsaidia nani?
  • Nimetumia muda mwingi kutengeneza au kutazama?
Majibu ya maswali haya yataonyesha kama unaondoka ndani ya Matrix au unaendelea kuishi ndani yake.

Uhuru Una Gharama

Kuvunja Matrix hakutakufanya upendwe na kila mtu. Utaitwa wa ajabu kwa sababu husikii kila taarifa mpya. Utaonekana nyuma kwa sababu hukimbilii kila mtindo mpya. Wengine watashangaa kwa nini unasoma vitabu wakati wao wanatazama video. Lakini baada ya miaka michache, matokeo yatazungumza kwa niaba yako. Wao watakuwa na kumbukumbu za video walizotazama. Wewe utakuwa umejenga maarifa, biashara, afya na tabia ambazo hazipotei kwa kubonyeza kitufe.

Matrix huanguka pale unapochagua kusudi badala ya starehe, maarifa badala ya kelele, na nidhamu badala ya msisimko wa muda mfupi.
Msingi wa mawazo ya sura hii umetokana na kazi za waandishi na wanafalsafa mbalimbali, wakiwemo:
  • Atomic Habits — James Clear.
  • Deep Work — Cal Newport.
  • Digital Minimalism — Cal Newport.
  • The Enchiridion — Epictetus.
  • Meditations — Marcus Aurelius.
  • The 7 Habits of Highly Effective People — Stephen R. Covey.
  • Man's Search for Meaning — Viktor E. Frankl.