TONE LA LAANA:SURA YA TANO
Tone la Laana
Unyayo wa viatu vizito vya kijeshi ulisikika ukipiga chini kwa nidhamu ya hali ya juu. Siku tatu baada ya vipimo vya Daktari Miller kuzua tafrani, serikali ya kikoloni pamoja na uongozi wa juu wa Kanisa ziliweka nguvu ya pamoja kufanya uchunguzi wa dharura. Hakukuwa na nafasi ya kubahatisha; kashfa hii iligusa misingi ya imani na sheria.
Kiongozi wa timu hiyo ya upelelezi alikuwa Inspector Thomas, afisa mwandamizi aliyetoka makao makuu ya polisi. Thomas alikuwa mhitimu wa mbinu za kijeshi za Scotland Yard, mtu mwenye uwezo wa kipekee wa kusoma alama na mazingira ambazo jicho la kawaida lisingeweza kuziona. Kwake yeye, "muujiza" ulikuwa ni neno linalotumiwa na watu waliofeli kufikiri kisayansi.
"Afisa Thomas, hapa ni mahali pa maombi na utawa. Hakuna jinai iliyofanyika hapa," Mama Mkuu Sista Celina alimweleza afisa huyo kwa sauti yenye mchanganyiko wa wasiwasi na msimamo.
"Sista," Inspector Thomas alijibu kwa sauti ya utulivu lakini yenye mamlaka makubwa, huku akivua glasi zake na kuzipangusa, "Sheria ya Fizikia na Biolojia haibadiliki kwa sababu ya kuta za monasteri. Kila athari ina chanzo. Kama kuna ujauzito bila muingiliano wa moja kwa moja wa kimwili, basi kuna njia ya pili iliyotumika. Na jukumu langu ni kuipata njia hiyo."
Thomas hakuanza kwa kuwahoji watu; alianzia kwenye kurejesha upya matukio (*Crime Scene Reconstruction*). Aliamuru bafu la masista, eneo la kisima, na mabanda ya mifugo vifungwe rasmi na kuwekwa chini ya ulinzi wa askari.
Akiwa ameshika kioo cha kukuzia picha (*magnifying glass*) na daftari lake dogo, Thomas alitembea hatua kwa hatua katika eneo la bafu la mbao. Alipiga magoti na kuanza kuchunguza kuta za mbao za bafu hilo.
"Kanuni ya Kwanza ya Upelelezi wa Kijeshi: Locard's Exchange Principle," Thomas alinong'ona peke yake. "Kila mguso huacha alama. Mtuhumiwa hawezi kupita mahali bila kuacha kitu au kuondoka na kitu."
Macho yake makali yalitua kwenye mbao za ukuta wa nyuma wa bafu—ukuta unaotenganisha bafu na eneo la kazi za nje. Aligundua kitu ambacho kila mtu alikuwa amekipuuza: kulikuwa na nafasi ndogo sana ya mianya iliyosababishwa na mbao kupasuka kutokana na jua na baridi. Zaidi ya hayo, kwenye udongo wa nje wa eneo hilo, Thomas aliona alama za viatu ambavyo havikuwa vya masista wala vya madaktari.
Alichukua rula na kupima kina cha udongo uliokanyagwa.
"Mtu huyu alikuwa amesimama hapa kwa muda mrefu. Hakupita tu—alikuwa amezubaika," Thomas alimweleza msaidizi wake, Corporal John. "Tazama presha yakisigino kwenye udongo huu. Mtu huyu alikuwa na wasiwasi au alikuwa akifanya kitendo kinachohitaji nguvu za mwili akiwa amesimama sehemu moja."
Mbinu iliyofuata ilikuwa ni Uchunguzi wa Saikolojia ya Tabia (*Behavioral Profiling*). Thomas aliwakusanya wafanyakazi wote wa nje—ikiwa ni pamoja na wale wanaotunza bustani na mifugo. Hakutaka kuwahoji kwa kuwatishia; alitumia mbinu ya kijeshi ya kutambua msukumo wa ndani wa mtuhumiwa (*Stress Signals*).
Wafanyakazi wote walipangwa mstari. Thomas alitembea mbele yao taratibu, akiwa ametuliza macho yake kwenye nyuso zao, mikono yao, na mifumo yao ya upumuaji.
"Tunachunguza muujiza au jinai," Thomas alisema kwa sauti ya juu na ya polepole. "Dawa ya kisasa ina uwezo wa kugundua chembe za damu na maji ya mwili hata kama yameoshwa na maji mengi. Yeyote aliyetupa kitu chochote ndani ya ndoo za maji za masista katika miezi miwili iliyopita, sayansi itamtaja kabla ya jua kuzama leo."
Hayo yalikuwa maneno ya mtego wa kisaikolojia (*Psychological Trap*). Thomas alijua fika kuwa teknolojia ya DNA ilikuwa bado haijafika kiwango hicho mwaka 1934, lakini alitumia utaalamu wa kisaikolojia kuleta hofu kwa mhusika halisi.
Papo hapo, jicho la Thomas lilimkamata Kassim!
Kassim alianza kupua pumzi kwa kasi, midomo yake ikakauka, na vidole vyake vya mikono vikaanza kutetemeka bila yeye kujua—viashiria vya wazi vya mwili kuitikia hofu kubwa ya ndani (*Fight or Flight Response*). Huku wenzake wakionyesha kushangazwa na maneno ya afisa huyo, Kassim pekee ndiye aliyekuwa akitazama chini, akijaribu kuficha macho yake.
"Wewe kijana," Thomas alimnyoshea kidole Kassim kwa utulivu wa kutisha. "Sogea mbele hatua tatu."
Kassim alitetemeka, miguu ikikosa nguvu. "A-Afisa... mimi... mimi sijafanya kitu..."
"Sijakuuliza kama umefanya kitu," Thomas alitabasamu kwa baridi, akimsogelea na kumtazama moja kwa moja machoni. "Leta mikono yako juu. Kucha zako zinaonyesha ulikuwa ukifanya kazi ya kusafisha mabanda, lakini vumbi lililopo kwenye viatu vyako ni udongo mwekundu wa upande wa bafu za masista—udongo ambao haupatikani upande wa nguruwe. Kwa nini viatu vyako vina udongo wa eneo ambalo hupaswi kukanyaga?"
Mtego wa kipelelezi ulikuwa umenasisha mawindo! Kassim alihisi pumzi zikimmfika mwisho, huku Thomas akiendelea kumwekea ushahidi mmoja baada ya mwingine uliomzunguka kama wavu wa chuma!