VIFURUSHI SABA
VIFURUSHI SABA
Hadithi ya kusisimua kutoka Maarifa360.
Jua lilikuwa linaelekea kuzama taratibu, likiacha mwanga wa dhahabu juu ya mji mzuri uliopambwa na nyumba za kisasa na bustani zilizotunzwa vizuri.
Barabarani alionekana msichana mmoja mrembo aitwaye Faraja akitembea kwa haraka. Masikioni alikuwa amevaa earphone huku kichwa chake kikitikisika taratibu kufuata mdundo wa wimbo aliokuwa akisikiliza.
Watu walikuwa wakipishana naye lakini hakuwajali. Mawazo yake yalikuwa mbali.
Upande wa pili wa barabara, mwanamke mmoja alimwangalia kwa jicho la husuda. Alimtazama kuanzia kichwani mpaka miguuni kisha akageuza uso wake kwa hasira.
Ghafla...
Sauti ya ajabu ilisikika mbele yake.
Sauti: Kwaaaah!
Faraja alishtuka na kusimama kwa sekunde chache.
Aligeuka kushoto na kulia.
Hakukuwa na mtu.
Alitikisa kichwa na kuendelea kutembea.
Dakika chache baadaye alifika kwenye nyumba ndogo ya kupanga. Alitoa funguo mfukoni, akafungua mlango na kuingia ndani.
Ndani kulikuwa kimya.
Kimya cha upweke.
Alivua viatu haraka, akatupa mkoba wake mkubwa kwenye kona ya chumba kisha akajitupa kitandani kwa uchovu.
Masikioni bado alikuwa amevaa earphone.
Mkono mmoja ulikuwa umeshika simu huku mwingine ukipiga piga kitandani kufuata mdundo wa muziki.
Kwa muda mfupi alionekana kusahau shida zote za maisha.
Lakini...
Ghafla sauti ya mtu ilisikika nje.
Tuma: Dadaaa! Dadaaa!
Faraja hakusikia.
Sauti ikaongezeka.
Tuma: Dadaaaa!
Bado hakusikia.
Nje ya mlango, kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi na miwili alikuwa akipiga kelele huku machozi yakimtoka.
Tuma: We dada! Funguaaaa!
Alijilaza juu ya mlango huku akilia kwa uchungu.
Dakika chache baadaye Faraja alisimama kwa uvivu, akaondoa earphone moja sikioni.
Faraja: Mbona kuna kelele?
Alisogea hadi mlangoni na kuufungua.
Puuuu!
Tuma aliangukia ndani kama gunia la mahindi.
Miguu yake ikapaa juu huku uso wake ukigonga sakafu.
Faraja alibaki amesimama akimwangalia.
Faraja: Hivi wewe ni kaka wa aina gani? Mbona huna akili kabisa?
Tuma alijinyanyua taratibu.
Akiwa bado amekaa chini alimuangalia dada yake.
Kisha...
Prrrrrr!
Alijamba.
Faraja alipanua macho kwa mshangao.
Tuma akatabasamu kwa aibu.
Tuma: Tatizo umerudi hata hujala, ukajifungia ndani.
Kisha akaanza kulia.
Faraja alishindwa kujizuia.
Alicheka.
Faraja: Haya basi kaka yangu mzuri. Asante kwa kujali.
Lakini safari hii Tuma hakutabasamu.
Uso wake ulijaa huzuni.
Tuma: Sio hivyo bwana.
Aliinama.
Tuma: Tunaishi kama wanyama.
Faraja akanyamaza.
Tuma: Nyumba moja hatuonani mpaka wiki nzima.
Kauli hiyo ilimgusa moja kwa moja moyoni.
Tuma: Utajiri sio hivyo. Familia kwanza.
Faraja alibaki kimya kwa sekunde kadhaa.
Maneno yale yalikuwa madogo, lakini yalikuwa mazito kuliko mawe.
Polepole alimvuta mdogo wake na kumkumbatia.
Faraja: Kaka yangu mpenzi... niambie leo umekula nini?
Tuma akajitoa mikononi mwake.
Kisha akaanza kuimba kwa sauti ya kulalamika.
Tuma: Njaa! Njaa! Nimekula njaaa!
Faraja akashika kichwa.
Tuma: Baba anatoka alfajiri nimelala. Anarudi usiku nipo nakoroma. Mama katukimbia. Wewe kukuona mpaka nivunje mlango. Bado unaniuliza nimekula nini?
Faraja alihisi macho yake yakianza kulowa.
Faraja: Tuma...
Tuma: Tuma nini? Basi nimekula mate.
Tuma akanyoosha ulimi.
Faraja akageuka haraka ili asione machozi yaliyokuwa yanataka kumtoka.
Alisogea kwenye mkoba wake.
Akautoa noti ya shilingi elfu moja.
Kisha akamkabidhi mdogo wake.
Faraja: Chukua hii.
Tuma aliitazama kana kwamba amepewa milioni moja.
Faraja: Kimbia gengeni kabla giza halijaingia. Kale viazi.
Uso wa Tuma ukang'aa kwa furaha.
Aligeuka tayari kukimbia.
Lakini kabla hajafika mlangoni...
Faraja alimvuta shati.
Faraja: Usichelewe kurudi. Ukirudi nenda moja kwa moja chumbani kwako ukalale. Usiniamshe. Nimechoka sana leo.
Tuma: Sawa dada.
Kisha akatoka mbio.
Mlango ulifungwa.
Kimya kikarudi tena ndani ya nyumba.
Faraja alirudi kitandani.
Akakaa.
Mawazo mengi yakaanza kumjia.
Maneno ya mdogo wake yalikuwa yakirudia rudia kichwani mwake.
Tuma: Tunaishi kama wanyama...
Tuma: Familia kwanza...
Polepole akajilaza akiwa bado amevaa nguo zake za kazi.
Muziki uliokuwa ukipiga kwenye simu ukapungua taratibu.
Macho yake yakaanza kufumba.
Lakini kabla hajalala...
Alihisi kama kuna mtu alikuwa amesimama nje ya dirisha akimtazama.
Faraja akafumbua macho kwa ghafla.
Hakukuwa na mtu.
Au labda...
Alikuwa yupo?
Mwili wake ulisisimka.
Akapinduka upande mwingine.
Ndani ya dakika chache usingizi mzito ukamchukua.
Bila kujua kwamba usiku huo ungekuwa mwanzo wa siri kubwa ambayo ingebadilisha maisha yake milele...
Maoni ya Wasomaji
Maoni yataonekana hapa kama comments zimewashwa kwenye post hii.
Andika Comment