SEHEMU YA PILI

Sehemu ya Pili - Vifurushi Saba
Hadithi

SEHEMU YA PILI – VIFURUSHI SABA

Safari ya Faraja inaanza kuingia kwenye siri nzito zaidi.

Faraja alishtuka kutoka usingizini kwa hofu kubwa.

Moyo wake ulikuwa ukidunda kwa kasi kana kwamba unataka kuruka kutoka kifuani.

Alifumbua macho taratibu.

Kilichokuwa mbele yake hakikuwa chumba chake.

Hakukuwa na kitanda.

Hakukuwa na ukuta.

Hakukuwa na mlango.

Alikuwa amelala katikati ya pori kubwa lililofunikwa na ukungu mzito.

Faraja: Nini hiki?

Haraka alianza kujikagua mwili wake.

Gauni alilovaa lilikuwa chakavu.

Miguu yake ilikuwa imejaa matope.

Ghafla macho yake yakatua kiunoni.

Kamba nene zilikuwa zimefungwa mwilini mwake.

Alizifuata kwa macho.

Mwisho wa kamba hizo kulikuwa na vifurushi saba vikubwa vilivyokuwa vinaburutwa ardhini.

Faraja: Aaaaaah! Mungu wangu! Nipo wapi mimi?

Aligeuka upande mwingine.

Macho yake yakakutana na mwili wa Tuma aliyekuwa amelala chini.

Faraja: Tuma! Tuma mdogo wangu!

Kwa furaha na hofu alijaribu kukimbia kumfuata.

Lakini...

Alipiga hatua moja tu.

Mzigo uliokuwa umefungwa mwilini mwake ulimvuta nyuma kwa nguvu.

Puuuu!

Alianguka vibaya.

Kishindo hicho kilimshtua Tuma.

Naye akafumbua macho.

Kwa sekunde kadhaa alitazama miti mirefu iliyowazunguka.

Kisha akamwangalia dada yake.

Tuma: Dada... sisi tupo wapi?

Faraja hakujibu.

Alikuwa analia.

Machozi yalikuwa yanamtoka bila kujizuia.

Tuma alimkaribia haraka.

Kisha akashika moja ya kamba zilizokuwa zimefungwa mwilini mwa dada yake.

Tuma: Ngoja nikusaidie.

Alivuta.

Ghafla mikono yake ikajaa damu.

Tuma: Aaaaa!

Aliruka nyuma kwa mshangao.

Faraja naye akapiga kelele.

Damu ilikuwa inatoka moja kwa moja ndani ya mwili wake.

Kana kwamba vifurushi vile vilikuwa sehemu ya mwili wake.

Kimya kizito kilitanda.

Kisha...

Sauti ya kutisha ilisikika nyuma yao.

Twaaaa!

Wote wawili waligeuka.

Mtu mmoja alikuwa amesimama umbali wa mita chache.

Alikuwa amevaa mavazi ya ajabu yaliyofanana na magunia.

Mkono mmoja ulikuwa umeshika fimbo ndefu.

Uso wake haukuonekana vizuri kutokana na ukungu.

Upepo mkali ukaanza kuvuma.

Majani yakaanza kuzunguka miguuni mwao.

Kadiri mtu huyo alivyosogea ndivyo hofu ilivyozidi.

Tuma alianza kutetemeka.

Faraja akajifunika uso kwa mikono.

Mtu huyo alifika mbele yao.

Hakusema neno.

Alinyoosha fimbo yake.

Kisha akaigusa paji la uso la Faraja.

GIZA.

Na ghafla, kila kitu kikabadilika...

Faraja alijikuta mahali pengine.

Alikuwa mgahawani.

Mikono yake ilibeba sinia lenye chai.

Alikuwa akiwahudumia wateja.

Jasho lilikuwa linamtoka.

Uso wake ulikuwa umechoka.

Ghafla sauti kali ilisikika.

Mwanamke: Muhudumuuuu!

Wateja wote waligeuka.

Faraja naye akageuka.

Mwanamke mmoja alikuwa ameketi pembeni.

Macho yake yalijaa hasira.

Faraja alimsogelea kwa heshima.

Faraja: Samahani mama, naweza kukuhudumia?

Mwanamke alicheka kwa dharau.

Mwanamke: Mama yako mimi? Kwenye cheti changu cha kuzaliwa umeona jina langu?

Faraja aliumia lakini hakujibu.

Aliinama kwa heshima.

Faraja: Samahani sana.

Mwanamke akatikisa kichwa.

Mwanamke: Niletee chai ya rangi na maandazi mawili.

Faraja alikimbia jikoni.

Baada ya muda akarudi na agizo.

Aliweka mezani kwa heshima.

Faraja: Kunahuduma nyingine unahitaji?

Mwanamke: Ndio.

Mwanamke alisimama.

Alichukua kikombe cha chai.

Na bila onyo...

Akamwaga chai yote kifuani mwa Faraja.

Faraja: Aaaaa!

Kisha mwanamke akamsukuma.

Faraja alianguka chini.

Wateja wote walibaki wakitazama.

Mwanamke: Jifunze kuwa makini! Mpumbavu wewe!

Faraja alianza kulia.

Lakini kabla mwanamke hajampiga...

Ulimwengu mzima ukapasuka.

Ghafla walikuwa porini tena.

Mwanamke yuleyule alikuwa amesimama mbele yao.

Faraja alibaki ameduwaa.

Faraja: Nini kinaendelea?

Mwanamke alinyanyua mkono.

Lakini kabla hajampiga...

Fimbo ilizuia mkono wake.

Mtu wa Ajabu alikuwa amesimama katikati yao.

Mtu wa Ajabu: Hapana. Amekushinda.

Mwanamke alirudi nyuma kwa hofu.

Mtu wa Ajabu akacheka.

Mtu wa Ajabu: Ondoka!

Tuma akakunja ngumi.

Tuma: Usimchezee dada yangu!

Akakimbia kuelekea kwa mwanamke.

Mtu wa Ajabu akamgusa kwa fimbo.

Prrrrrr!

Tuma akajamba.

Kisha akaanguka chini kama gunia.

Mtu wa Ajabu akatikisa kichwa.

Mtu wa Ajabu: Huyu bado mdogo.

Faraja alimwangalia kwa mshangao.

Mtu huyo akatoa kisu.

Akainama.

Kisha akakata kamba mbili zilizokuwa zimefungwa kwenye mwili wa Faraja.

Mara moja.

Vifurushi viwili vikadondoka chini.

Ukungu ukatikisika.

Ardhi ikaanza kutetemeka.

Mwanamke akapiga kelele kali.

Mwanamke: Aaaaaaaaah!

Alishika kifua.

Akapiga magoti.

Macho yake yakaanza kupoteza mwanga.

Mwili wake ukaanguka chini.

Kimya.

Hakutikisika tena.

Alikuwa amekufa.

Faraja alirudi nyuma kwa hofu.

Faraja: Hii ni nini? Sielewi.

Mtu wa Ajabu akamwangalia.

Kisha akasema kwa sauti ya mamlaka:

Mtu wa Ajabu: Mwanangu... marafiki wana nguvu sana, hasa wanapokufundisha mambo mabaya.

Faraja alinyamaza.

Mtu huyo akaendelea.

Mtu wa Ajabu: Dunia ni paradiso. Shida si dunia. Shida ni Zambi Kuu.

Faraja akakunja uso.

Faraja: Zambi Kuu ni nini?

Mtu wa Ajabu akatazama vifurushi vilivyobaki.

Kisha akasema:

Mtu wa Ajabu: Hizi ndizo. Hizi ndizo zinazoleta umasikini. Hizi ndizo zinazoleta hofu. Hizi ndizo zinazoleta chuki. Hizi ndizo zinazoleta mateso.

Faraja akatazama vifurushi vitano vilivyobaki.

Kwa mara ya kwanza alihisi uzito wake.

Faraja: Naweza kuviondoa vipi?

Mtu wa Ajabu akacheka.

Mtu wa Ajabu: Dunia weeeh... Dunia ni tamu sana. Shida ni kwamba shetani anakuchukia.

Faraja akakasirika.

Faraja: Wewe nani hasa?

Mtu huyo akageuka.

Ukungu ukafunika uso wake.

Kisha akatabasamu.

Mtu wa Ajabu: Mimi? Mimi ni Mtu wa Ajabu.

Na mbali kabisa porini...

Sauti ya kitu kisichojulikana ilisikika.

Kana kwamba kilikuwa kinawatafuta.

Mtu wa Ajabu akashtuka.

Uso wake ukabadilika.

Mtu wa Ajabu: Tayari wamejua tupo hapa. Harakeni! Msisimame!

Faraja akatazama nyuma.

Katikati ya ukungu...

Kulikuwa na macho mekundu mawili yakitazama upande wao.

Mwili wake wote ukasisimka.

Safari ya kweli ilikuwa ndiyo kwanza inaanza...

Inaendelea...

Usikose Sehemu ya Tatu ya hadithi hii hapa Maarifa360.

Soma Sehemu ya Tatu

Umeipenda makala hii? Washirikishe wengine kupitia WhatsApp.

Share WhatsApp

Maoni ya Wasomaji

Maoni yataonekana hapa kama comments zimewashwa kwenye post hii.

Andika Comment