Tone la Laana

TONE LA LAANA - Sura ya Kwanza
Tone la Laana Cover

Tone la Laana

Mwandishi: Evarist Mimitu
SURA YA KWANZA: MAUA YA MILIMA YA USAMBARA

Msomaji wangu, ili uweze kuelewa uzito wa machozi yatakayomwagika baadaye katika kuta hizi za mawe, ni lazima kwanza ukanyage ardhi ya baridi ya Gare, iliyopo juu kabisa katika Milima ya Usambara, mkoani Tanga, mwaka wa Bwana 1934.

Eneo hili lilikuwa kama bustani ya Edeni. Ukungu mzito wa asubuhi ulikuwa ukitanda juu ya misitu ya minazi na misonobari, huku hewa safi na ya baridi ikipuliza kwa utulivu. Katika bonde hilo la utulivu, lilimsimama jengo kubwa la mawe ya matofali mekundu—Monasteri ya Bikira Maria Imakulata.

Humo ndani, alikuwepo binti mmoja aliyekuwa na tabasamu lililoweza kuyeyusha hata moyo ulioshikwa na barafu. Jina lake aliitwa Clare.

Kabla ya kuvaa shela nyeupe na kuapa kiapo cha maisha ya utawa, Clare alikuwa binti wa Mzee Kibena, mwalimu wa kwanza wa katekisimu katika eneo lote la Lushoto. Clara alikuwa mrembo ajabu. Macho yake makubwa ya mviringo yalitazama kwa huruma, na ngozi yake ya rangi ya shaba iliteleza kama iliyopakwa mafuta ya nyonyo. Vijana wengi matajiri wa kijiji, akiwemo mtoto wa Chifu aliyekuwa na ng'ombe mamia, walipiga hodi nyumbani kwa Mzee Kibena wakimtaka Clara awe mke wao.

Lakini Clara alikuwa na msimamo mmoja tu tangu akiwa msichana mdogo wa miaka kumi na mbili: Moyo wake ulikuwa mali ya Yesu Kristo.

"Baba," Clara alimwambia Mzee Kibena siku aliyogonga miaka kumi na nane, "dunia ina mambo mengi ya kunishawishi, lakini amani yangu ninaiona katika kumtumikia Mungu. Nataka kuwa sista."

Mzee Kibena, ingawa alitamani kupata wakwe na wajukuu, alipiga magoti na kumbariki binti yake wa pekee.

✦ ✦ ✦

Siku aliyoingia monasteri kuanza mafunzo ya usista (unovisi), Clara hakuwa peke yake. Alikuwa pamoja na rafiki yake wa damu tangu utotoni, binti mmoja aliyeitwa Bernadette—au 'Berny' kama Clare alivyopenda kumwita kwa siri.

Bernadette alikuwa tofauti kabisa na Clare. Wakati Clare alikuwa tulivu, mpole na mwenye kupenda kusali masaa mengi, Bernadette alikuwa kama moto wa kifuu—mwenye mhemko, mcheshi, na aliyekuwa na uwezo wa kuchekesha hata mawe ya monasteri!

"Clare myangu," Bernadette alinong'ona siku yao ya kwanza kufika monasteri, wakiwa wamepiga magoti kwenye kanisa dogo la maombi, huku watawa wakubwa wakiwa wamefumba macho kwa umakini. "Hivi kweli tutaweza kuvumilia maisha haya? Tazama magoti yangu... tayari yameshaanza kuwa meusi kama sufuria la maharagwe kwa sababu ya kupiga magoti saa sita mchana!"

Clare alijitahidi kubana mdomo wake usicheke kwa sauti, lakini sauti ya Bernadette ilikuwa ikimvunja mbavu.

"Nyamaza Berny, Masista waandamizi watatusikia!" Clare alinong'ona huku akijaribu kutazama mbele kwa umakini.

"Sikiliza Clare," Bernadette aliendelea kunong'ona kwa sauti ya chini huku akipenyeza kipande cha mihogo ya kuchoma alichokuwa amekificha kwenye mfuko wa kanzu yake. "Mimi naingia usista kwa sababu mbili tu: Kwanza, sitaki kuolewa na wale wanaume wa kijijini kwetu wenye ndevu kama mbuzi wazee. Pili, naipenda sana hiyo shela nyeupe! Lakini masuala ya kuamka saa kumi za usiku kwenye baridi hii ya Usambara... Mungu mwenyewe anajua natumia imani ya ziada!"

Clare alishindwa kujizuia, alitoa kicheko kidogo cha chini. Mama Mkuu wa Nyumba, Sista Celina—mwanamke wa Kizungu mwenye sura iliyojaa ukali na nidhamu ya Kijerumani—aligeuka na kuwakodolea macho makali yaliyowafanya wote wawili wakaze nyuso zao papo hapo na kujifanya wako kwenye maombi mazito.

Bernadette alikuwa ndiye furaha na kichocheo cha Clare. Katika vipindi vya kazi ngumu kama kulima bustani, kuosha vyombo, au kufanya usafi wa majengo, Bernadette ndiye aliyekuwa akileta visa vya kuvunja mbavu vilivyowafanya mabinti hao wavumilie maisha magumu ya kutaabisha mwili ili kuitakasa roho.

✦ ✦ ✦

Miaka mitatu ya mafunzo ilipita kwa kasi. Clare alionekana kuwa mtawa wa mfano—mnyenyekevu, mwenye upendo kwa kila mtu, na aliyeshika sheria zote za Kanisa bila kunung'unika.

Hatimaye, siku kubwa ikawadia. Siku ya Kuweka Nadhiri za Daima.

Kanisa kuu la monasteri lilipambwa kwa maua meupe ya milimani. Harufu ya ubani ilitanda hewani. Askofu Mkuu wa Jimbo la Tanga alikuwa amesimama mbele ya altare, akiongoza Misa Takatifu. Clara—sasa akiitwa rasmi Sista Maria Clare—alikuwa amelala kifudifudi mbele ya altare, kama ishara ya kufa kwa ulimwengu na kufufuka katika maisha ya Kristo.

Alipoinuka, alivalishwa shela nyeupe kichwani na pete ya fedha kidoleni. Moyo wake ulifurika amani isiyo na kifani. Alihisi amefikia kilele cha furaha ya maisha yake.

"Mungu wangu," Sista Clare alinong'ona kwa sauti ya ndani kabisa akiwa amepiga magoti mbele ya sanamu ya Bikira Maria. "Kuanzia leo, mimi ni wako. Mwili wangu, roho yangu na maisha yangu yote ni yako. Naomba unilinde katika usafi huu hadi siku nitakapokutana nawe Mbinguni."

Pembeni yake, Bernadette—ambaye naye sasa alikuwa Sista Bernadette—alimkonyeza jicho moja kwa furaha, ingawa alikuwa akijipepea kwa kitambaa kwa sababu ya joto la mishumaa.

Kila mtu aliamini Sista Clare alikuwa malaika aliyetumwa duniani. Kila sista alimpenda, na wote waliona usafi na utakatifu ukimulika usoni pake.

Lakini hakuna hata mmoja wao—wala Sista Clare mwenyewe, wala Sista Bernadette, wala Mama Mkuu Sista Celina—aliyedhani kuwa chini ya milima hiyo ya Usambara, dhoruba nzito ilikuwa ikijikusanya.

Dhoruba ambayo ingekuja kutikisa sio tu Monasteri ya Gare, bali msingi mzima wa Kanisa Katoliki nchini Tanganyika. Na chanzo cha dhoruba hiyo, kilikuwa kikianzia katika eneo dogo sana la monasteri hiyo... eneo la banda la nguruwe!