KANUNI 20-SURA TANO
Biashara Imara Hujengwa kwa Nidhamu, Sio Bahati
Baada ya kulinda mtaji dhidi ya matumizi mabaya, mikopo isiyo na tija na maamuzi ya haraka, hatua inayofuata ni kujenga mfumo unaofanya biashara idumu kwa miaka mingi. Wafanyabiashara wengi wanaofanikiwa kwa muda mfupi huanguka kwa sababu hawakuwa na nidhamu ya kuendesha biashara. Fedha zinaingia, lakini hazitengenezi msingi wa kesho.
KANUNI YA TISA
Dhibiti Matumizi Madogo Kabla Hayajawa Makubwa
Wafanyabiashara wengi hufuatilia hasara za mamilioni lakini hawafuatilii matumizi ya elfu kumi au elfu ishirini yanayotokea kila siku. Ndiyo matumizi hayo madogo yanayomeza mtaji polepole.
Safari zisizo za lazima, mafuta yasiyodhibitiwa, vocha za simu, posho zisizo na utaratibu, bidhaa zinazotolewa bure bila sababu na matumizi ya starehe huonekana madogo. Lakini baada ya miezi kadhaa vinaweza kuwa sawa na mtaji wa kuongeza biashara.
Mmiliki wa duka la vifaa vya umeme alikuwa anatoa fedha kidogo kidogo kila siku kwa matumizi ambayo hakuyaandika popote. Alipofanya tathmini mwisho wa mwaka aligundua zaidi ya shilingi milioni saba zilikuwa zimetumika kwenye matumizi ambayo hayakuongeza hata mteja mmoja. Fedha hizo zingetosha kufungua tawi jipya.
KANUNI YA KUMI
Usiue Faida kwa Vita ya Bei
Wafanyabiashara wengi huamini njia pekee ya kupata wateja ni kushusha bei kuliko kila mtu mwingine. Hili ni kosa kubwa. Ukianza kushindana kwa bei pekee, siku zote kutakuwa na mtu mwenye uwezo wa kushusha zaidi kuliko wewe.
Badala ya kushusha bei, ongeza thamani. Toa huduma bora. Jibu simu haraka. Fikisha bidhaa kwa wakati. Toa dhamana. Mteja anayeheshimu ubora mara nyingi hachagui bei ya chini kabisa.
Maduka mawili yaliuza bidhaa zinazofanana. Duka la kwanza lilishusha bei kila wiki. Duka la pili lilibaki na bei yake lakini lilitoa huduma bora, ushauri wa kitaalamu na huduma ya kufikisha bidhaa kwa wateja. Baada ya mwaka mmoja, duka la kwanza lilikuwa linapata wateja wengi lakini halikuwa na faida. Duka la pili lilikuwa na wateja wachache lakini faida yake ilikuwa kubwa zaidi.
KANUNI YA KUMI NA MOJA
Ajiri Polepole, Ondoa Tatizo Mapema
Mfanyakazi mzuri huongeza thamani ya biashara. Mfanyakazi asiye mwaminifu hupunguza faida kila siku. Anaweza kuiba bidhaa, kuharibu mahusiano na wateja, kutoa siri za biashara au kufanya makosa yanayokugharimu fedha nyingi.
Usiajiri kwa sababu tu una haraka. Fanya mahojiano vizuri. Kagua historia yake. Mfundishe utamaduni wa biashara yako. Na ukigundua mtu anaharibu biashara kwa makusudi, chukua hatua mapema. Kuchelewa kufanya maamuzi ya uongozi ni gharama nyingine inayokula mtaji.
- Hufanya bajeti kila mwezi.
- Hufuatilia matumizi kila siku.
- Hachukui fedha za biashara kiholela.
- Hajishughulishi na mashindano ya kuonyesha utajiri.
- Hutengeneza mfumo, si kutegemea bahati.