SEHEMU YA TATU
VIFURUSHI SABA - JARIBU
Faraja anakutana na jaribu jipya, lakini safari hii msaada unaanza kupotea.
Ukungu mzito ulikuwa bado umetanda porini.
Faraja, Tuma na Mtu wa Ajabu walikuwa wakitembea kwa tahadhari katikati ya miti mirefu.
Hakuna aliyekuwa akizungumza.
Kila mmoja alikuwa amezama kwenye mawazo yake.
Faraja alikuwa akivuta vifurushi vilivyobaki nyuma yake kwa shida. Kila hatua aliyopiga iliacha alama ndefu ardhini.
Tuma alikuwa akitembea pembeni yake, mara akijaribu kubeba kifurushi kimoja, mara akikimbilia kingine, lakini kila alipokigusa alihisi kama mikono yake inachomwa moto.
Mtu wa Ajabu alikuwa mbele yao, fimbo yake ikiwa mkononi, macho yake yakitazama huku na kule kama mtu anayejua hatari iko karibu.
Ghafla...
Harufu tamu ya nyama choma ilianza kusikika hewani.
Tuma alisimama.
Pua yake ilianza kufanya kazi kuliko kawaida.
Tuma: Nasikia harufu ya pilau...
Akakunja uso.
Tuma: Kuku wa kukaanga pia.
Akavuta pumzi tena kwa nguvu.
Tuma: Na samaki!
Faraja alimtazama kwa hasira kidogo.
Faraja: Tuma, acha mchezo. Hapa si sehemu ya kufikiria chakula.
Tuma alishika tumbo lake.
Tuma: Dada, mimi nikisikia harufu ya chakula akili yangu inakuwa na mkutano wa dharura.
Mtu wa Ajabu hakusema chochote.
Aliendelea kutembea.
Muda mfupi baadaye walifika kwenye eneo la wazi.
Walichokiona mbele yao kiliwafanya wote wasimame.
Katikati ya eneo hilo kulikuwa na meza kubwa iliyopambwa kwa vyakula vya kila aina.
Kulikuwa na pilau, nyama choma, kuku, samaki, matunda, keki, juisi, na chupa za pombe za bei ghali zilizopangwa kama mapambo ya kifalme.
Meza ile haikuonekana kama meza ya porini.
Ilikuwa kama meza ya sherehe ya watu matajiri.
Mbele ya meza hiyo aliketi mzee mmoja wa makamo.
Alikuwa akila kwa madaha, polepole, huku akicheka mwenyewe kana kwamba dunia yote ilikuwa mali yake.
Macho ya Tuma yakatanuka.
Tuma: Ooooh My God!
Akakimbia kuelekea mezani.
Lakini kabla hajagusa hata kipande cha nyama...
Zaaap!
Mwanga wa ajabu ulimpiga mwilini.
Tuma alirushwa nyuma kama mpira.
Prrrrrr!
Akajamba kwa nguvu.
Kisha akaanguka chini akigalagala.
Tuma: Aaaah! Hii nyama ina ulinzi?
Aliinuka kwa hasira.
Tuma: Leo nitakupiga!
Alitaka kumvamia mzee.
Lakini Mtu wa Ajabu alimzuia kwa ishara ya mkono.
Tuma akasimama, akakaa kimya, lakini bado alikuwa akimtazama mzee kwa macho ya chuki na njaa.
Mzee akatabasamu.
Tabasamu lake lilikuwa la kinafiki.
Mzee: Karibu Faraja.
Mzee: Kaa upate chakula cha kifalme.
Faraja akamtazama Mtu wa Ajabu.
Mtu wa Ajabu akatikisa kichwa taratibu.
Kana kwamba alimruhusu.
Faraja akasogea mezani.
Tuma akafoka.
Tuma: Yaani utakula peke yako? Nasi je?
Akajaribu kukaa kwenye kiti kingine.
Lakini...
Zaaap!
Alipigwa shoti nyingine.
Safari hii akaanguka chini na kupoteza fahamu.
Faraja akashtuka.
Alitaka kukimbia kumfuata.
Lakini Mtu wa Ajabu akamzuia.
Mtu wa Ajabu: Muache.
Mtu wa Ajabu: Ataamka.
Mtu wa Ajabu: Wewe kula.
Mzee akatafuna kipande cha nyama huku akitabasamu.
Mzee: Naona Baba yenu anawalinda sana.
Faraja akakunja uso.
Faraja: Huyu si baba yangu.
Mzee akacheka kwa dharau.
Mzee: Kimwili si baba yako.
Mzee: Lakini kifkra?
Akamtazama Mtu wa Ajabu kwa dharau.
Mzee: Huoni jinsi anavyokupigania?
Kisha uso wake ukabadilika.
Mzee: Lakini safari hii lazima ashindwe.
Mzee: Njaa uliyo nayo ni kubwa sana.
Faraja alitazama meza tena.
Ni kweli alikuwa na njaa.
Tangu jana usiku hakujua hata kama alikuwa amekula sawasawa.
Harufu ya chakula ilimchanganya.
Kila kitu mezani kilionekana kinamuita.
Mtu wa Ajabu akasema kwa msisitizo:
Mtu wa Ajabu: Kula Faraja.
Mtu wa Ajabu: Unahitaji nguvu kuyashinda majaribu.
Mzee akamtazama Faraja kwa macho makali.
Faraja akanyamaza kwa muda.
Kisha badala ya kujipakulia kwanza, alichukua maji.
Akasogea kwa Mtu wa Ajabu.
Akamnawisha mikono.
Mtu wa Ajabu alimtazama bila kusema neno.
Faraja akachukua sahani.
Akapakua chakula kidogo sana.
Akamkabidhi Mtu wa Ajabu.
Kisha akachukua sahani nyingine.
Akapakua chakula kidogo tena.
Akaenda alikolala Tuma.
Akamwamsha taratibu.
Faraja: Tuma, amka. Kula kidogo.
Tuma alifumbua macho kwa shida.
Alipoiona sahani, nguvu zilimrudia ghafla.
Faraja akamnawisha mikono.
Kisha akampa chakula.
Tuma akafakamia kama mtu aliyekuwa hajala wiki nzima.
Tuma: Dada, huu ndio upendo wa kweli.
Alijiramba vidole.
Mzee aliyekuwa mezani alianza kubadilika uso.
Hasira zikaanza kuonekana machoni mwake.
Faraja akarudi mezani.
Akajipakulia chakula kidogo sana.
Akala taratibu.
Hakuharakisha.
Hakuchukua zaidi.
Baada ya muda mfupi akaweka sahani chini.
Faraja: Asante sana. Nimetosheka.
Kimya kikatanda.
Mzee akasimama ghafla.
Uso wake ulikuwa umejaa hasira.
Mzee: Kula!
Mzee: Faraja, kula chakula!
Faraja akashtuka.
Lakini hakugusa tena chakula.
Mzee akapiga meza kwa mikono yake.
Vyombo vikatetemeka.
Chupa zikagongana.
Mzee: Unadhani unaweza kunishinda kwa kujifanya una kiasi?
Alinyanyua mkono.
Alitaka kumpiga Faraja kwa nguvu ile ile iliyompiga Tuma.
Lakini Mtu wa Ajabu akawahi.
Akaweka fimbo yake kifuani mwa mzee.
Mtu wa Ajabu: Muache.
Mtu wa Ajabu: Tafadhali muache.
Mtu wa Ajabu: Amekushinda.
Mzee akapiga kelele za maumivu.
Damu ikaanza kumtoka mdomoni.
Lakini bado alimtazama Faraja kwa chuki.
Mzee: Nakuapia...
Mzee: Nitamsakama kila atakapokwenda.
Mzee: Na siku moja nitamshinda.
Mtu wa Ajabu hakujibu.
Alitoa kisu.
Akamtupia Tuma.
Mtu wa Ajabu: Tuma!
Mtu wa Ajabu: Kata kamba mbili.
Mtu wa Ajabu: Ziondoe kwa dada yako haraka.
Mtu wa Ajabu: Kisha zichukue umfunge huyu mzee.
Tuma alipokea kisu kwa mikono inayotetemeka.
Tuma: Mimi tena?
Mtu wa Ajabu alimwangalia tu.
Tuma akameza mate.
Tuma: Sawa, nimeelewa.
Akakimbia kwa Faraja.
Akakata kamba mbili.
Vifurushi viwili vikadondoka chini.
Mara moja Faraja alihisi mwili wake kuwa mwepesi zaidi.
Alipumua kwa nguvu.
Kama mtu aliyekuwa amebeba dunia mgongoni.
Tuma akachukua kamba zile.
Akaanza kumfunga mzee kwa haraka.
Mzee alipiga kelele kwa hasira.
Wakati huo Mtu wa Ajabu akamgeukia Faraja.
Mtu wa Ajabu: Faraja, ondoka.
Mtu wa Ajabu: Kimbia haraka.
Faraja akamtazama.
Faraja: Na Tuma?
Mtu wa Ajabu: Usisimame. Kimbia.
Faraja akageuka.
Akapiga hatua moja.
Ya pili.
Ya tatu.
Ghafla...
Ulimwengu ukabadilika.
Alijikuta peke yake katika eneo jingine la pori.
Vifurushi vitatu pekee vilikuwa vimebaki mwilini mwake.
Aligeuka nyuma.
Hakumuona Tuma.
Hakumuona Mtu wa Ajabu.
Hakumuona mzee.
Alikuwa peke yake.
Lakini upande mwingine...
Mzee aliyekuwa akifungwa alianza kucheka.
Kicheko chake kilikuwa cha kutisha.
Mzee: Sim sala bim...
Mzee: Sim sala bim...
Mzee: Sim sala bim...
Ghafla ardhi ilitikisika.
Ukungu ukazunguka kila mahali.
Mtu wa Ajabu na Tuma wakatoweka.
Walipozinduka walijikuta ndani ya chumba kidogo kisicho na mlango.
Chumba kilikuwa kitupu.
Kuta zake zilijaa michoro ya ajabu.
Tuma akaanza kulia.
Tuma: Dada amekwisha!
Mtu wa Ajabu akamweka mkono begani.
Mtu wa Ajabu: Usilie.
Mtu wa Ajabu: Wewe ni Tumaini.
Tuma akamtazama kwa macho yaliyokuwa yamejaa machozi.
Mtu wa Ajabu akaendelea:
Mtu wa Ajabu: Tuombe Mungu hekima imtawale Faraja.
Mtu wa Ajabu: Kwa sababu sasa...
Alinyamaza kwa sekunde chache.
Kisha akatazama juu.
Mtu wa Ajabu: Sasa ni muda wake wa kujiongoza mwenyewe.
Na kwa mara ya kwanza tangu safari hii ianze...
Faraja alikuwa peke yake.
Hakukuwa na Mtu wa Ajabu.
Hakukuwa na Tuma.
Mbele yake kulikuwa na mlango mkubwa mweusi.
Mlango ambao hakuwahi kuuona maishani mwake.
Juu yake kulikuwa na maneno yaliyoandikwa kwa rangi nyekundu kama damu:
JARIBU LA TATU
Mwili wa Faraja ulisisimka.
Akavuta pumzi ndefu.
Kisha akaanza kuusogelea mlango huo taratibu...
Bila kujua nini kilikuwa kinamsubiri upande wa pili.
Maoni ya Wasomaji
Maoni yataonekana hapa kama comments zimewashwa kwenye post hii.
Andika Comment