FITINA ZA BIASHARA-SURA YA 1
Biashara ni Vita Visivyo na Bunduki
Fitina Za Biashara
Abdallah alikuwa ameanza biashara ya vifaa vya ujenzi kwa mtaji mdogo sana. Miaka mitatu baadaye alikuwa ameongeza wateja, akaajiri wafanyakazi watano na biashara yake ikaanza kujulikana mjini. Alidhani changamoto yake kubwa ilikuwa kupata mtaji zaidi. Kumbe changamoto halisi ilikuwa kulinda mafanikio aliyokuwa ameyapata.
Siku moja mteja wake mkubwa alimjulisha kuwa ameamua kununua bidhaa kwa muuzaji mwingine. Hakukuwa na tatizo la ubora wala bei. Kilichokuwa kimetokea ni kwamba mtu alikuwa amemwambia kuwa Abdallah anauza bidhaa feki na kwamba biashara yake ilikuwa karibu kufungwa. Habari hizo zilikuwa za uongo, lakini zilitosha kumfanya mteja huyo aogope.
Ndipo Abdallah aligundua ukweli ambao wafanyabiashara wengi huuchelewa kuujua. Kadiri biashara yako inavyokua, ndivyo watu wanaotamani nafasi yako wanavyoongezeka.
Ushindani wa Haki na Ushindani wa Fitina
Kuna ushindani mzuri ambao kila mfanyabiashara anatamani kuuona. Mtu anaboresha huduma, anashusha gharama za uzalishaji, anaongeza ubunifu na anawahudumia wateja vizuri zaidi. Ushindani huu huifanya soko likue na wateja wanufaike.
Lakini pia kuna ushindani usio wa haki. Hapa lengo si kuwa bora kuliko mpinzani wako. Lengo ni kuhakikisha mpinzani hafiki mbali hata kama bidhaa yako si bora kuliko yake.
Katika ushindani huu ndipo huzaliwa fitina nyingi. Zingine ni ndogo kiasi kwamba huwezi kuzitambua mapema. Zingine ni kubwa kiasi kwamba zinaweza kufunga biashara ndani ya wiki chache.
Kwa Nini Fitina Huongezeka Kadiri Biashara Inavyokua?
Biashara inayokua huvutia macho ya watu wengi. Baadhi yao ni wateja wapya. Baadhi ni wawekezaji. Lakini wengine ni washindani wanaotafuta kujua umefanikiwaje ili wakuzuie usiendelee kukua.
Usishangae mtu aliyekuwa hakujui kabisa aanze kukuomba umweleze supplier wako, mfumo wako wa bei, idadi ya wateja wako au faida unayopata kila mwezi. Maswali hayo yanaweza kuonekana ya kawaida, lakini wakati mwingine ndiyo mwanzo wa ujasusi wa biashara.
Usimwambie kila mtu kila kitu kuhusu biashara yako.
Taarifa ni mali. Ukiitoa ovyo, unaweza kumpa mshindani silaha ya kukushinda.
Biashara Inahitaji Ulinzi Kama Inavyohitaji Mauzo
Wafanyabiashara wengi hutumia muda mwingi kutafuta wateja lakini hutumia muda mdogo kulinda biashara zao. Huweka nguvu kwenye matangazo lakini husahau usalama wa taarifa, mikataba, mifumo ya fedha na wafanyakazi.
Fikiria nyumba nzuri yenye milango wazi usiku kucha. Uzuri wa nyumba hauwezi kuzuia mwizi kuingia. Vivyo hivyo, biashara yenye bidhaa nzuri lakini isiyo na mfumo wa kujilinda huwa rahisi kushambuliwa.
Ndiyo maana kampuni kubwa duniani huwekeza fedha nyingi kwenye mikataba, sheria, usalama wa taarifa, ukaguzi wa ndani na mafunzo ya wafanyakazi. Wanajua kuwa kulinda biashara ni sehemu ya kuikuza.
Katika sura zinazofuata utajifunza fitina zinazotumiwa mara nyingi dhidi ya wafanyabiashara, dalili zake, sababu zinazozifanya zitokee na mbinu za kujilinda bila kuvunja sheria wala maadili. Lengo si kukuogopesha, bali kukufanya uwe mfanyabiashara mwenye tahadhari, anayelinda kile anachokijenga kila siku.