FITINA ZA BIASHARA - SURA YA 3

SURA YA TATU

Fitina za Ndani

Adui wa Hatari Zaidi Anaweza Kuwa Ndani ya Kampuni Yako

Wafanyabiashara wengi huamini kuwa adui mkubwa yupo nje ya biashara yao. Hiyo si kweli kila wakati. Mara nyingi biashara huanza kudhoofika kutoka ndani, taratibu sana, mpaka siku moja mmiliki anashangaa fedha zimepungua, wateja wameondoka na siri za biashara zipo mikononi mwa washindani.

Biashara nyingi hazifi kwa shambulio moja kubwa. Hufa kwa makosa madogo yanayorudiwa kila siku na watu waliopo ndani ya kampuni.

Ukuta wa nje unaweza kuwa imara. Lakini ufa mdogo wa ndani unaweza kuangusha jengo lote.

Fitina ya Kwanza: Mfanyakazi wa Siri

Siyo kila anayefanya kazi kwako ana ndoto ya kuona biashara yako ikikua. Wapo wanaokuja kujifunza mfumo wako, kukusanya taarifa zako na kujenga mahusiano na wateja wako kabla hawajaondoka kuanzisha biashara inayofanana na yako au kuhamia kwa mshindani.

Hii haimaanishi kuwa kila mfanyakazi ni mbaya. Lakini mfanyabiashara mwenye busara hujenga mfumo unaolinda biashara hata pale mfanyakazi mzuri anapoamua kuondoka.

Dalili za Tahadhari
  • Anataka kujua kila taarifa hata zisizomhusu.
  • Anawasiliana sana na washindani.
  • Anaanza kuficha taarifa muhimu.
  • Anabadilika ghafla bila sababu.
  • Anakusanya taarifa za wateja kupita kiasi.

Fitina ya Pili: Wizi Unaotabasamu

Wizi mkubwa wa biashara mara nyingi hauanzi kwa mamilioni. Huanza na kiasi kidogo kisichoonekana. Fedha kidogo leo, bidhaa moja kesho, taarifa muhimu kesho kutwa. Baada ya miezi kadhaa hasara huwa kubwa sana.

Ndiyo maana ukaguzi wa mara kwa mara ni muhimu hata kama unaamini kila mtu ndani ya kampuni yako.

Linda Mfumo Badala ya Kutegemea Uaminifu Pekee.

Watu wazuri wanaweza kubadilika. Lakini mfumo mzuri hubaki kuwa mfumo mzuri.

Fitina ya Tatu: Mteja Anaibiwa Taratibu

Baadhi ya wafanyakazi huanza kujenga mahusiano binafsi na wateja wa kampuni. Baadaye wanapoondoka, wanaondoka pia na orodha ya wateja. Ghafla biashara yako inaanza kupoteza mauzo huku ukijiuliza kilichotokea.

Mteja anatakiwa kuifahamu kampuni yako kwanza, si mfanyakazi mmoja pekee.

Fitina ya Nne: Siri za Kampuni Kutoka Nje

Quotation, bei za bidhaa, mikataba, supplier, mishahara ya wafanyakazi na mikakati ya biashara ni mali muhimu. Zikivuja kwa washindani, wanaweza kupanga hatua zao kwa kutumia taarifa zako mwenyewe.

Taarifa ni mali. Mali isiyolindwa huwa zawadi kwa mshindani.

Fitina ya Tano: Wabia Wasiowasiliana

Biashara nyingi huanza kwa urafiki. Lakini zinapokua, maamuzi yanakuwa magumu zaidi. Bila mawasiliano ya wazi, wabia huanza kutuhumiana. Hapo ndipo migogoro huanza.

Fedha zinapokuwa nyingi, urafiki pekee hauwezi kulinda biashara. Lazima kuwe na mfumo, uwazi na kumbukumbu sahihi.

Kanuni ya Dhahabu

Usijenge biashara inayotegemea mtu mmoja. Jenga biashara inayotegemea mfumo. Mfumo mzuri huendelea kufanya kazi hata watu wakibadilika.

Katika sura inayofuata utaona jinsi wabia, wawekezaji na hata marafiki wanaweza kugeuka kuwa chanzo cha migogoro mikubwa ya biashara ikiwa makubaliano hayakuwekwa wazi tangu mwanzo.