KANUNI 20-SURA YA NNE

SURA YA NNE

Fedha Hupotea Kimya Kimya Kabla Biashara Haijafilisika

Biashara nyingi hazianguki kwa tukio moja kubwa. Mara nyingi huanza kuvuja kidogo kidogo. Leo ni matumizi yasiyo na mpango. Kesho ni bidhaa zilizolala ghalani. Keshokutwa ni mteja mmoja anayechukua sehemu kubwa ya mapato. Mmiliki haoni hatari kwa sababu kila tatizo linaonekana dogo. Lakini yanapoungana, huondoka na mtaji wote.

Hasara kubwa huanza na matumizi madogo yaliyopuuzwa.

KANUNI YA SITA

Usikimbilie Kila Fursa Inayong'aa

Kila wiki kuna mtu atakuambia kuna biashara mpya inalipa sana. Wengine watakushawishi uache biashara uliyoijenga kwa miaka kadhaa uingie kwenye mradi ambao hata haujaufanyia utafiti. Mfanyabiashara mwenye busara hachanganyiki na kila upepo wa biashara. Anaelewa kuwa mafanikio yanatokana na umakini, si kubadilisha mwelekeo kila mwezi.

Mfano – Mbeya

Bakari alikuwa na duka la pembejeo za kilimo lililokuwa linaendelea vizuri. Baada ya kusikia watu wakizungumza kuhusu biashara ya cryptocurrency, alitoa sehemu kubwa ya mtaji wake akawekeza bila kuelewa mfumo wake. Msimu wa kilimo ulipofika hakuwa na fedha za kuongeza bidhaa dukani. Wateja wake walihamia maduka mengine. Alipopoteza fedha kwenye uwekezaji mpya, aligundua alikuwa ameharibu biashara iliyokuwa tayari inamlipa.

KANUNI YA SABA

Hesabu Zako Ndizo Macho ya Biashara

Biashara ambayo haina taarifa sahihi za mapato na matumizi ni sawa na dereva anayefunga macho halafu anaendesha gari kwa kasi. Usikubali kufanya biashara kwa kukisia. Jua kila siku: Mapato yamekuwa kiasi gani? Faida ni kiasi gani? Gharama zimeongezeka kwa nini? Ni bidhaa gani zinauza zaidi? Ni bidhaa gani zimekwama ghalani?

Tabia ya Wafanyabiashara Wanaofanikiwa:
  • Hufanya hesabu kila siku.
  • Hukagua Cash Flow kila wiki.
  • Hukagua faida kila mwezi.
  • Hufanya tathmini ya biashara kila robo mwaka.
Biashara inapimwa kwa namba, si kwa hisia.

KANUNI YA NANE

Usimtegemee Mteja Mmoja Pekee

Wafanyabiashara wengi hufurahia kupata mteja mmoja mkubwa anayenunua karibu kila kitu. Lakini siri ambayo wengi hawaijui ni kwamba mteja huyo anakuwa na nguvu kubwa kuliko mwenye biashara. Akiondoka, biashara inaweza kuporomoka ndani ya mwezi mmoja. Lengo lako liwe kuwa na wateja wengi wanaonunua kidogo kidogo kuliko mmoja anayenunua kila kitu.

Mfano – Kampuni ya Usambazaji

Kampuni moja ilikuwa inauza zaidi ya asilimia sabini ya bidhaa zake kwa shule moja binafsi. Shule ilipobadilisha msambazaji baada ya miaka mitatu, mapato ya kampuni yalishuka ghafla. Walilazimika kupunguza wafanyakazi na kufunga matawi mawili. Tatizo halikuwa kupoteza mteja. Tatizo lilikuwa kutegemea mteja mmoja.
Mteja mmoja anaweza kukuinua. Lakini wateja wengi ndiyo wanaifanya biashara idumu.