LAANA YA FAMILIA SURA YA TATU
SURA YA TATU: UMASKINI NA MAHUSIANO YANAYORITHIWA
Juma alikuwa kijana mwenye bidii ya ajabu. Alipambana kusoma, akapata kazi nzuri katika kampuni ya kimataifa, na kwa mara ya kwanza katika historia ya familia yao, akaanza kupata mshahara mkubwa. Ndugu zake walishangilia; ilionekana kana kwamba umaskini uliokuwa umeikumba familia yao kwa miaka sitini hatimaye ulikuwa umefika mwisho.
Lakini miaka mitano baadaye, Juma alikuwa amezama kwenye madeni ya kinyonyaji. Kila mara alipoweka akiba kidogo, lilitokea "dharura" ya kifamilia, biashara ya upande aliyoianzisha ilifeli kwa njia za kijinga, au alijikuta akitumia fedha kwa vitu visivyo na tija ili tu kuwaridhisha watu wengine. Alipoketi usiku mmoja na kuangalia akaunti yake ya benki iliyokuwa haina kitu, alishtuka. Alikuwa anaishi maisha yale yale ya baba yake mzazi—mtu aliyefanya kazi kwa miaka 30 lakini akafa akiwa hana hata kiwanja.
Je, familia ya Juma ilirogwa? Au kuna mfumo usioonekana uliokuwa ukimvuta kurudi chini kila alipojaribu kuinua kichwa?
Fikiria kisa cha Neema. Kila mara alipofikisha akiba ya shilingi milioni tano kwenye akaunti yake, ubongo wake ulianza kujisikia vibaya. Alijisikia hatia kuwa na fedha wakati mama yake na dada zake wanateseka. Bila kujua, alikuwa anatafuta njia ya "kujikwamua" kutoka kwenye hatia hiyo kwa kuikopesha fedha hiyo watu ambao alijua fika hawatamrudishia. Ndani ya miezi mitatu, alirudi tena sifuri. Mfumo wake wa fahamu ulitulia tu pale aliporudi kwenye hali ya 'uhaba'—hali iliyokuwa inajulikana na kuzoeleka na familia yake.
Dk. Bessel van der Kolk, katika kitabu chake cha "The Body Keeps the Score," anaeleza jinsi mazingira ya dhiki ya muda mrefu yanavyobadilisha mfumo wa fahamu wa mwanadamu. Mtu aliyekulia katika umaskini uliokithiri anajenga mfumo wa fahamu unaoendeshwa na hali ya 'Kujilinda na Dharura' (Survival Mode). Kwake yeye, fedha si chombo cha uwekezaji au ustawi wa muda mrefu, bali ni kitu cha kutatulia dharura ya leo kabla haijatoweka.
Pia, mtaalamu Anne Ancelin Schützenberger kupitia kitabu chake cha "The Ancestor Syndrome," anaeleza dhana ya "Hatia ya Mafanikio" (Loyalty Guilt). Mjumbe wa familia anapofanikiwa kuliko wengine wote, anajikuta akipambana na msukumo wa ndani usioonekana unaomwambia: "Huna haki ya kuwa na furaha au utajiri wakati damu yako inateseka." Hali hii inamfanya afanye maamuzi mabaya ya kifedha ili tu kurudi kwenye kiwango cha kawaida cha ukoo.
Kama vile umaskini unavyoweza kuwa mzunguko wa kizazi, ndivyo ilivyo kwa mahusiano ya kimapenzi na ndoa. Mfano wa kawaida katika jamii yetu ni binti anayekua akishuhudia mama yake akipigwa, kutelekezwa, au kutukuzwa na baba yake. Binti huyu anakua akiahidi kwa uchungu: "Sitawahi kuolewa na mwanamume mwenye tabia kama za baba yangu."
Lakini anapofikisha umri wa mahusiano, anajikuta anavutiwa na mwanamume ambaye mwanzoni anaonekana mpole, lakini miezi michache baada ya kuoana, anaanza kuonyesha tabia zile zile za ukali, udhibiti, na ukatili wa kihisia. Ni kwa nini hii hutokea?
Amina alilelewa na baba aliyekuwa na tabia ya kutoweka nyumbani na kumfanya mama yake alie kila usiku. Amina alipokuwa mtu mzima, alipata waombaji wengi wa ndoa. Mwanamume wa kwanza alikuwa mpole, mwenye kujali, na alimthamini sana, lakini Amina alihisi "hakuna msisimko" (no chemistry). Mwanamume wa pili alikuwa wa baridi, asiyetabirika, na aliyempa majeraha ya kihisia—Amina alijikuta akimkimbilia huyu wa pili kwa nguvu zote. Kwa nini? Kwa sababu akili yake ya subconscious ilitafsiri 'hangaiko la kihisia' kuwa ndiyo maana halisi ya upendo.
Dr. Lindsay C. Gibson, katika kitabu chake mashuhuri cha "Adult Children of Emotionally Immature Parents," anafafanua jambo hili kwa kina sana. Mtoto anapokulia katika mikono ya wazazi waliokosa ukomavu wa kihisia (emotionally immature parents), anajenga mtazamo kwamba ili kupendwa, lazima ujitese, ujipendekeze, au uvumilie maumivu. Akili ya mwanadamu naturally inavutiwa na kile kinachojulikana (the familiar), hata kama kile kinachojulikana kinatesa.
Mtaalamu wa saikolojia ya uchanganuzi Galit Atlas, katika kitabu chake cha "Emotional Inheritance," anaeleza kwamba maumivu ya kihisia ambayo hayakutatuliwa katika kizazi kimoja yanatafuta 'jukwaa' la kujirudia katika kizazi kinachofuata.
Pia, Mark Wolynn katika kitabu cha "It Didn't Start with You," anatukumbusha kuwa mzunguko wa kuvunjika kwa ndoa au migogoro ya kifamilia mara nyingi hutokana na 'Kukatika kwa Mnyororo wa Upendo' (Interrupted Bonding Trigger). Mzazi ambaye hakuwahi kupendwa au kulindwa na wazazi wake, anakuwa na ugumu mkubwa wa kutoa upendo wa dhati na salama kwa watoto wake au kwa mwenza wake. Matokeo yake, anajenga ukuta wa kujilinda unaosababisha migogoro isiyoisha.
Iwe ni mzunguko wa umaskini usioelezeka au mnyororo wa ndoa zenye mateso na kuvunjika, lazima tuelewe ukweli mmoja mzito: Huu si uchawi wa kurogwa kwenye pembe za nyumba; ni ramani ya kisaikolojia tuliyorithi na kuanza kuisafiria bila kuikagua.
Huatakiwi kuendelea kuwa mtumwa wa ramani uliyokabidhiwa. Hatua ya kwanza ya kuvunja mzunguko huu si kukimbilia kwa waganga au kukaa na kulalama; ni kusimama imara, kuangalia ukweli bila hofu, na kusema: "Mnyororo huu wa umaskini na maumivu ya mahusiano unaishia kwangu."