UZIO WA UBINAFSI-SURA YA 4

SURA YA 4

Kanuni za Kunusurika

UZIO WA UBINAFSI: Jinsi ya Kunusurika Katika Dunia Inayokuangalia Ukiangamia

Mwandishi: Ivan Mahimbi

Baada ya kujua kuwa dunia haitakuonya kila mara, na baada ya kuelewa kuwa maoni ya wengi yanaweza kukubeba mpaka mahali usipotaka kufika, sasa kinachobaki si malalamiko. Kinachobaki ni kujenga mfumo wako wa kujilinda.

Maisha ya sasa hayamhurumii mtu asiye na kanuni. Ukiishi bila kanuni, utaishi kwa kusukumwa na watu, mitandao, presha ya jamii, tamaa, hofu, hasira na hali ya muda. Leo utataka ndoa kwa sababu watu wameoa. Kesho utataka kuacha ndoa kwa sababu watu wanalalamika. Leo utataka kuacha kazi kwa sababu mtu ameongea kwa kujiamini mtandaoni. Kesho utataka kurudi kuajiriwa kwa sababu biashara imekuchapa.

Mtu asiye na kanuni ni kama nyumba isiyo na mlango. Kila mtu anaweza kuingia, kuweka kitu chake, kuondoka, na kukuacha ukibeba mizigo ambayo si yako.

Usipojijengea kanuni zako, dunia itakupa kanuni zake; na nyingi hazikutengenezwa kukuokoa.

Kanuni ya Kwanza: Usifanye Uamuzi Mkubwa Ukiwa Ndani ya Hisia Kubwa

Moja ya makosa makubwa ya maisha ni kufanya uamuzi wa kudumu ukiwa kwenye hisia ya muda. Hasira inapokuja, akili hupungua. Hofu inapokuja, maono yanapungua. Furaha kubwa inapokuja, tahadhari hupungua. Wivu unapokuja, mtu huanza kushindana na watu ambao hata hawajui anashindana nao.

Usiache kazi kwa hasira ya bosi. Usiingie kwenye ndoa kwa presha ya umri. Usivunje uhusiano kwa sababu rafiki zako wamekusukuma siku moja. Usikope fedha kwa sababu unaona aibu kuonekana huna. Usiweke siri zako zote kwa mtu kwa sababu umemzoea ndani ya wiki mbili.

Hisia zinaweza kuwa za kweli, lakini si kila hisia ni mshauri mzuri.

Kabla ya uamuzi mkubwa, jiulize: je, bado nitaamua hivi kesho nikiwa mtulivu? Je, ningeamua hivi kama hakuna mtu anayenishinikiza? Je, nitaweza kubeba matokeo ya uamuzi huu nikibaki peke yangu?

Kanuni ya vitendo: Uamuzi wowote mkubwa unaogusa ndoa, kazi, biashara, fedha, kuhama, kuacha kitu, au kuanza jambo kubwa usifanywe ndani ya saa 24 za hasira, wivu, hofu au msisimko mkubwa.

Kanuni ya Pili: Usichukue Ushauri wa Maisha Kutoka kwa Mtu Ambaye Huwezi Kutaka Maisha Yake

Kuna watu wengi wanaongea vizuri kuliko wanavyoishi. Wanaweza kukupa ushauri mzito kuhusu ndoa wakati wao hawajawahi kujenga uhusiano wenye afya. Wanaweza kukufundisha biashara wakati hawajawahi kubeba hasara halisi. Wanaweza kukuambia uache kazi wakati wao wanaishi kwa msaada wa watu wengine.

Hii haimaanishi kuwa mtu lazima awe mkamilifu ndiyo akushauri. Hakuna mtu mkamilifu. Lakini angalau angalia mwelekeo wa maisha yake. Angalia matunda ya maamuzi yake. Angalia kama ana nidhamu kwenye eneo analokushauri.

Mtu aliyeshindwa jambo anaweza kukufundisha kitu muhimu ikiwa amejifunza kutokana na kushindwa kwake. Lakini mtu aliyeshindwa halafu hajajifunza, mara nyingi atakupa hasira zake badala ya hekima.

Usipokee ushauri kwa sababu mtu anaongea kwa nguvu. Pokea ushauri kwa sababu unaona msingi wa hekima nyuma ya maneno yake.

Kanuni ya Tatu: Jenga Watu Watatu wa Ukweli

Katika dunia iliyojaa watu wanaoogopa kukuambia ukweli, unahitaji watu wachache wenye ruhusa ya kukukwaza kwa ajili ya kukulinda. Si watu wengi. Watu watatu tu wanaweza kutosha kama ni wa kweli.

Mtu wa kwanza awe mtu mwenye hekima kuliko wewe. Mtu anayejua maisha kwa kina, si kwa maneno ya mtandaoni. Mtu ambaye anaweza kuona mbali kuliko hisia zako.

Mtu wa pili awe mtu anayekujua vizuri. Anayejua historia yako, udhaifu wako, tabia zako na namna unavyobadilika ukiwa kwenye hatari.

Mtu wa tatu awe mtu asiyehitaji kitu kutoka kwako. Mtu ambaye hatakuogopa kwa sababu ya cheo, fedha, umaarufu au hasira yako.

Wape ruhusa. Waambie wazi: “Ukiona naelekea pabaya, niambie. Hata nikikasirika, usiache kuniambia.”

Mtu asiye na mtu wa kumwambia ukweli anaweza kuzungukwa na watu wengi lakini akawa mpweke kiakili.

Kanuni ya Nne: Chunguza Kabla ya Kuamini

Karne hii ina taarifa nyingi kuliko hekima. Kila siku kuna wazo jipya, biashara mpya, mfumo mpya, dawa mpya, fursa mpya, njia mpya ya kupata pesa, na ushauri mpya wa maisha. Ukiamini kila kitu kwa haraka, utachoka kabla hujajenga chochote.

Usipochunguza, utakuwa mteja wa kila kelele.

Mtu akikuambia biashara fulani inalipa, usiulize faida tu. Uliza gharama. Uliza hasara. Uliza muda wa kurudisha mtaji. Uliza soko. Uliza ushindani. Uliza changamoto za wateja. Uliza waliowahi kujaribu wakashindwa.

Mtu akikuambia mahusiano yako hayafai, usiulize tu anaona nini. Uliza: je, anaongea kutokana na ushahidi au maumivu yake binafsi? Je, tatizo hili ni la kuvunja au la kurekebisha? Je, mimi mwenyewe nimefanya nini kulikuza?

Mtu akikuambia acha kazi, usimuulize tu atakavyokushangilia ukiacha. Muulize utakavyolipa kodi mwezi wa tatu kama biashara haijaenda.

Maswali matano kabla ya kuamini:
1. Chanzo cha taarifa hii ni nini?
2. Mtu huyu ana faida gani nikiamini?
3. Ni ushahidi gani unaounga mkono maneno yake?
4. Ni hatari gani hazisemwi?
5. Mimi ndiye nitakayebeba matokeo gani?

Kanuni ya Tano: Usijenge Maisha Kwa Kuogopa Maneno ya Watu

Maneno ya watu yamefanya watu wengi waishi maisha yasiyo yao. Mtu anaoa kwa sababu watu watasema amechelewa. Mtu anazaa kwa sababu watu watasema hana mtoto. Mtu ananunua gari kwa sababu watu watasema hajafanikiwa. Mtu anajenga nyumba kwa presha, si mpango. Mtu anaacha ndoto yake kwa sababu watu watamcheka.

Ukiishi kwa kuogopa watu watasema nini, utaishi kama mtumwa asiyeona minyororo yake.

Ni kweli, jamii ina nafasi yake. Maoni ya watu si ya kupuuzwa yote. Lakini maoni ya watu hayapaswi kuwa dira ya mwisho ya maisha yako.

Jiulize: kama hakuna mtu angejua, bado ningefanya hivi? Kama nisingepost, bado ningetaka hiki kitu? Kama watu wasingenipongeza, bado ningechagua njia hii?

Maswali haya yatakuonyesha kama unafanya jambo kwa sababu ni sahihi, au kwa sababu unataka kuonekana.

Kanuni ya Sita: Usiruhusu Upweke Ukuchagulie Maamuzi

Upweke ni mshauri hatari. Unapokuwa mpweke, mtu yeyote anayekupa umakini anaweza kuonekana kama zawadi. Unapokuwa mpweke, ujumbe mmoja unaweza kuonekana kama upendo. Unapokuwa mpweke, unaweza kubaki kwenye mahusiano yanayokuharibu kwa sababu unaogopa kurudi kwenye ukimya.

Upweke ukikuongoza, utakubali vitu ambavyo usingekubali ukiwa na amani ndani yako.

Jifunze kukaa na wewe mwenyewe. Jifunze kutengeneza maisha ambayo hayategemei mtu mmoja kukufanya ujisikie una thamani. Jifunze kujenga marafiki, kazi, ibada, afya, kusoma, na malengo binafsi.

Mtu aliye na maisha ya ndani yenye nguvu hachagui watu kwa njaa ya hisia. Huchagua kwa utulivu.

Usiingie kwenye mahusiano kwa sababu huwezi kukaa peke yako. Ingia kwa sababu umeona mtu anayefaa kuingia naye.

Kanuni ya Saba: Jua Tofauti Kati ya Kuvumilia na Kujidharau

Kuna mahali maisha yanahitaji uvumilivu. Kazi ngumu inahitaji uvumilivu. Ndoa yenye changamoto za kawaida inahitaji uvumilivu. Biashara inayokua polepole inahitaji uvumilivu. Kujifunza kitu kipya kunahitaji uvumilivu.

Lakini kuna mahali uvumilivu hugeuka kujidharau.

Ukimya wako ukianza kukumaliza, chunguza. Kusamehe kwako kukianza kuruhusu mtu arudie kukuumiza bila kubadilika, chunguza. Kuvumilia kwako kukianza kukuondolea utu, chunguza. Kukaa kwako mahali kukianza kukufanya ujichukie, chunguza.

Si kila kuondoka ni kushindwa. Wakati mwingine kuondoka ni kujilinda. Na si kila kubaki ni uaminifu. Wakati mwingine kubaki ni hofu iliyovaa nguo za uvumilivu.

Kanuni ya Nane: Usipende Kusifiwa Kuliko Kurekebishwa

Moja ya dalili za mtu anayeelekea kuharibikiwa ni kuchagua watu wanaomsifia tu. Anapenda kusikia kwamba yuko sahihi. Anapenda watu wanaokubali kila anachosema. Anapenda marafiki wanaompa makofi hata pale anapofanya ujinga.

Sifa nyingi bila marekebisho hujenga kiburi. Na kiburi kikikomaa, huanza kumfanya mtu aone kila onyo kama chuki.

Usijenge maisha yako kwenye kundi la watu wanaokupenda ukiwa unacheka tu. Tafuta pia watu wanaoweza kukaa nawe wakati unakosea na kukuambia, “Hapa unaenda vibaya.”

Ukichukia kila anayekurekebisha, siku moja utabaki na wanaokupamba mpaka uingie shimoni ukiwa unaonekana vizuri.

Kanuni ya Tisa: Jifunze Kuchelewesha Majibu

Si kila kitu kinahitaji ujibu mara moja. Si kila ujumbe unahitaji majibu ya haraka. Si kila lawama inahitaji kujitetea papo hapo. Wakati mwingine, nguvu yako iko kwenye kuchelewa kujibu mpaka akili itulie.

Ukiwa na hasira, maneno yako huwa na sumu nyingi kuliko busara. Ukiwa umeumizwa, unaweza kusema kitu ambacho baadaye kitakugharimu. Ukiwa umefurahi sana, unaweza kuahidi kitu ambacho hutaweza kutimiza.

Jifunze kusema, “Nitalifikiria.” Jifunze kusema, “Nitajibu baadaye.” Jifunze kusubiri usiku mmoja kabla hujatuma ujumbe wa hasira. Jifunze kuandika kile unachohisi, halafu usikitume mpaka akili irudi.

Kanuni ya saa moja: Ukipokea ujumbe unaokukasirisha sana, usijibu ndani ya saa moja ya kwanza. Ukijibu ukiwa umetulia, utajibu kwa akili zaidi kuliko jeraha.

Kanuni ya Kumi: Usichanganye Ujasiri na Mihemko

Watu wengi leo wanaita mihemko ujasiri. Mtu anaacha kazi bila mpango, anasema ana imani. Mtu anaingia kwenye biashara asiyoielewa, anasema ana uthubutu. Mtu anavunja uhusiano bila kutafakari, anasema amejitambua.

Ujasiri wa kweli haukimbii kufikiri. Ujasiri wa kweli unaangalia hatari, unaipima, unaandaa mbinu, kisha unaamua. Mihemko hukimbia kwanza na kufikiri baadaye.

Usijidanganye. Si kila hatua ya ghafla ni hatua ya imani. Wakati mwingine ni kukosa nidhamu ya kufikiri.

Ujasiri bila hekima unaweza kukupeleka mbali, lakini si lazima ukakufikisha salama.

Kanuni ya Kumi na Moja: Kagua Watu Unaowasikiliza Mara kwa Mara

Akili yako inafanana polepole na sauti unazoruhusu ziingie ndani yake. Ukisikiliza watu wenye hasira kila siku, utaanza kuona dunia kwa hasira. Ukisikiliza watu wenye tamaa kila siku, utaanza kuona kila kitu kama njia ya kujionyesha. Ukisikiliza watu wenye nidhamu, taratibu utaanza kuona thamani ya nidhamu.

Usichague tu chakula cha mwili. Chagua pia chakula cha akili.

Kagua accounts unazofuatilia. Kagua marafiki unaokaa nao muda mrefu. Kagua mazungumzo yanayokutawala. Kagua vitabu, video na makundi unayoingia. Kama kitu kinakufanya uwe na wivu, uchungu, hasira, tamaa au kuchukia maisha yako bila sababu, punguza nafasi yake.

Kanuni ya Kumi na Mbili: Jenga Maisha Yanayoweza Kubeba Ukweli

Kuna watu maisha yao yote yamejengwa kwenye uongo wa kuonekana. Wanaonekana wana pesa, lakini madeni yanawafukuza. Wanaonekana wana ndoa nzuri, lakini ndani kuna vita. Wanaonekana wana furaha, lakini hawawezi kukaa peke yao bila kuvunjika.

Ukiishi kwa kuonekana, ukweli utakuwa adui yako. Ukiishi kwa kujijenga, ukweli utakuwa mwalimu wako.

Usikubali maisha yako ya nje yakue kuliko maisha yako ya ndani. Usikubali picha zako ziwe bora kuliko tabia yako. Usikubali watu waamini umefika wakati wewe mwenyewe unajua hujaanza.

Jenga polepole. Jenga kweli. Jenga kwa msingi ambao hauhitaji uongo mwingi kuusimamia.

Kanuni ya Kumi na Tatu: Usifanye Kosa la Kudharau Dalili Ndogo

Kabla maisha hayajaharibika, mara nyingi huwa yanatoa dalili. Deni linaanza kidogo. Uhusiano unaanza kuvunjika kwa mazungumzo madogo yanayopuuzwa. Afya inaonyesha ishara ndogo. Tabia mbaya inaanza kama mzaha. Uzembe unaanza kama siku moja tu.

Watu wengi hawaharibiki kwa sababu dalili hazikuwepo. Huharibika kwa sababu walizipuuzia.

Usidharau tabia ndogo inayojirudia. Usidharau matumizi madogo yanayozidi kipato. Usidharau uongo mdogo unaokua. Usidharau maumivu ya mwili yanayorudi mara kwa mara. Usidharau ukimya unaoongezeka kwenye mahusiano.

Kanuni ya dalili: Kitu kidogo kinachojirudia si kidogo tena. Ni mfumo unaoanza kujengwa.

Kanuni ya Kumi na Nne: Andika Maamuzi Yako Makubwa

Kabla hujachukua uamuzi mkubwa, andika kwa nini unataka kufanya hivyo. Andika faida. Andika hatari. Andika vitu vitakavyoharibika. Andika mpango mbadala. Andika watu watakaoathirika.

Kuandika kunapunguza mihemko. Mawazo yanapobaki kichwani, yanaweza kuonekana makubwa kuliko yalivyo. Ukiyaweka kwenye karatasi, unaanza kuona ukweli wake.

Kama huwezi kueleza uamuzi wako kwa maandishi, huenda bado hujaufikiria vya kutosha.

Kanuni ya Kumi na Tano: Acha Kuomba Ruhusa kwa Watu Wanaofaidika na Udhaifu Wako

Kuna watu hawataki ubadilike kwa sababu wananufaika na wewe ukiwa dhaifu. Wengine wanapenda uwe tegemezi. Wengine wanapenda uendelee kuomba msaada. Wengine wanapenda uwe chini ili wajisikie wako juu.

Ukiwa unaomba ruhusa ya kukua kwa watu wanaonufaika na udogo wako, hutapewa baraka.

Jifunze kutambua watu wanaokuunga mkono unapolia, lakini wanakosa furaha unapoinuka. Watu hao si lazima uwachukie, lakini usiwape mamlaka ya kuamua hatua zako.

Kanuni ya Kumi na Sita: Weka Mipaka Kabla Hujachoka

Watu wengi huweka mipaka wakiwa wamechoka sana. Hapo mipaka yao huja kama hasira, ugomvi au kukata watu ghafla. Mipaka mizuri haipaswi kusubiri uchovu wa mwisho.

Weka mipaka kwenye muda wako. Weka mipaka kwenye fedha zako. Weka mipaka kwenye watu wanaokutumia. Weka mipaka kwenye mazungumzo yanayokuchafua. Weka mipaka kwenye mambo unayoweza kubeba na ambayo huwezi kubeba.

Kusema hapana si ukatili. Wakati mwingine ni njia ya kuendelea kuwa na amani ya kusema ndiyo mahali sahihi.

Mtu asiye na mipaka hugeuka uwanja wa kila mtu kupitishia mizigo yake.

Kanuni ya Kumi na Saba: Usipoteze Sauti Yako ya Ndani

Kila mtu ana sauti ya ndani inayomwonya kabla ya makosa makubwa. Wengine huiita dhamiri. Wengine huiita intuition. Wengine huiita hekima ya ndani. Jina si muhimu sana. Muhimu ni kwamba mara nyingi sauti hiyo huanza kunong’ona kabla maisha hayajapiga kelele.

Ukianza kusema moyoni, “Hapa kuna kitu hakiko sawa,” usipuuze haraka. Chunguza. Kama mtu anakupa ahadi kubwa sana lakini ndani yako kuna hofu isiyoelezeka, chunguza. Kama biashara inaonekana rahisi mno, chunguza. Kama uhusiano unakupa wasiwasi wa mara kwa mara, chunguza.

Dhamiri ikinyamazishwa mara nyingi, huanza kuongea kwa sauti ndogo. Usiiue kwa kuipuuza kila siku.

Mwisho wa Sura ya Nne

Kanuni hizi hazitafanya maisha yasiwe na matatizo. Hazitazuia watu kukaa kimya. Hazitazuia wengine kukupa ushauri mbaya. Hazitazuia mitandao kupiga kelele. Lakini zitakupa kitu muhimu zaidi: uwezo wa kusimama katikati ya kelele bila kupoteza mwelekeo.

Kuishi katika dunia yenye Uzio wa Ubinafsi kunahitaji mtu mwenye ulinzi wa ndani. Watu wanaweza kukuonya au wasikuonye. Wanaweza kukusaidia au wakakutazama. Wanaweza kukusifia au kukupotosha. Lakini ukiwa na kanuni, hautakuwa rahisi kubebwa na kila upepo.

Usisubiri dunia ikujengee uzio wa kukulinda. Jenga uzio wako wa hekima, nidhamu, watu wa ukweli, utashi na maamuzi yaliyofikiriwa.

Kwa sababu dunia inaweza kukutazama ukiangamia.

Lakini wewe huna ruhusa ya kujitazama ukiangamia bila kufanya chochote.