TULIKUTANA TENA-SURA YA 3
Reli ya Hatima
TULIKUTANA TENA: Mapenzi Yaliyoshinda Karne
Baada ya usiku wa daraja la reli, Margaret alifungiwa ndani ya nyumba kama ndege aliyekamatwa kabla hajajifunza kuruka mbali. Baba yake hakumpiga, hakupaza sauti sana, lakini alifanya jambo lililouma zaidi. Alimnyamazisha kwa ukimya mzito uliokuwa unaonekana kwenye kila kona ya nyumba.
Kwa siku tatu, Margaret hakuruhusiwa kwenda dukani, kanisani wala kutembea nje bila mama yake. Barua zake zote zilikusanywa. Baba yake alifungua sanduku lake, akatoa vipande vya karatasi alivyokuwa akiandika hadithi, akavisoma kwa macho ya hukumu, kisha akavitupa kwenye moto.
Margaret alisimama pembeni ya jiko, akitazama ndoto zake zikiteketea. Hakulia mbele yake. Alikuwa amejifunza kuwa machozi mbele ya mtu asiyejali huwa yanakuwa ushindi wake.
Usiku huo, mama yake aliingia chumbani kwake kimya kimya. Alikuwa amebeba kikombe cha chai na kipande kidogo cha mkate.
Mama yake: “Kula kidogo, mwanangu.”
Margaret: “Sina njaa.”
Mama yake: “Moyo ukiumia, mwili hujifanya hauna njaa. Lakini bado unahitaji nguvu.”
Margaret aliketi kitandani. Macho yake yalikuwa yamechoka, lakini ndani yake kulikuwa na kitu kilichokataa kufa.
“Mama,” alisema kwa sauti ndogo, “ulikuwahi kumpenda mtu ambaye dunia haikutaka umpende?”
Mama yake hakujibu mara moja. Alitazama dirishani, kwenye giza lililokuwa nje. Kwa sekunde chache, uso wake ulionekana kuwa wa msichana mwingine, si mama aliyekuwa amezoea kukaa kimya.
“Ndiyo,” alisema hatimaye. “Lakini nilichagua amani.”
“Na ulipata amani?”
Mama yake alifumba macho. “Nilipata maisha.”
Margaret alielewa tofauti ya maneno hayo mawili. Maisha na amani hayakuwa kitu kimoja.
Jonas Hakukata Tamaa
Upande wa pili wa mji, Jonas aliendelea kwenda karibu na duka la vitabu kila siku. Mzee Samuel alimwangalia kwa huruma kila alipoingia na kutoka bila jibu.
Siku ya nne, Samuel alimpa Jonas kitabu cha zamani. Jonas alikitazama bila kuelewa.
Jonas: “Sina fedha ya kununua kitabu leo.”
Samuel: “Sijasema ununue. Fungua ukurasa wa mwisho.”
Jonas alifungua. Ndani kulikuwa na karatasi ndogo iliyokunjwa. Mwandiko ulikuwa wa Margaret.
Jonas,
Wamechoma karatasi zangu, lakini hawajachoma kilichonifanya niandike. Wamenifungia ndani, lakini kila treni inapopita karibu na nyumba yetu, nahisi bado niko njiani. Usije karibu na nyumba. Baba yangu anasubiri kosa moja tu. Lakini usifikiri nimekusahau. Kama kunisubiri kutakuumiza, basi niache. Kama kunipenda kutakugharimu, basi fikiria tena. Mimi siwezi kukuahidi njia rahisi.
Margaret.
Jonas aliisoma barua hiyo mara nyingi mpaka karatasi ikaanza kulainika mikononi mwake. Mzee Samuel alimwangalia kimya kimya.
“Utamwacha?” mzee aliuliza.
Jonas aliikunja barua kwa uangalifu na kuiweka ndani ya koti lake.
“Mzee, watu hawaachi kupumua kwa sababu hewa ni baridi.”
Samuel alitabasamu kwa huzuni. “Basi uwe tayari. Mapenzi yanapogusa nyumba za wenye kiburi, huwa hayapiti bila damu.”
Pendekezo la Baba
Wiki moja baadaye, Bwana Whitmore alimuita Margaret sebuleni. Kulikuwa na mgeni. Mwanaume aliyeitwa Edward Harlan, mfanyabiashara kijana kutoka familia yenye mali. Alikuwa amevaa vizuri, alizungumza kwa adabu, na alimtazama Margaret kana kwamba alikuwa bidhaa nzuri iliyowekwa sokoni kwa wakati sahihi.
Margaret alijua kabla hata hawajasema. Baba yake alikuwa ameamua kumtafutia mume.
Edward alizungumza naye kuhusu hali ya hewa, vitabu na muziki. Alikuwa mpole, lakini upole wake haukugusa moyo. Alikuwa sahihi kwa kila kitu ambacho jamii ilitaka, na mgeni kabisa kwa kila kitu ambacho Margaret alihitaji.
Baada ya Edward kuondoka, baba yake alimwambia wazi.
Bwana Whitmore: “Edward ni kijana mzuri. Ana familia nzuri. Ana biashara inayokua.”
Margaret: “Mimi simpendi.”
Bwana Whitmore: “Mapenzi si msingi wa ndoa imara. Heshima, mali na jina ndizo msingi.”
Margaret: “Basi wewe unataka niolewe nyumba, si mtu.”
Baba yake alisimama kwa hasira, lakini hakumpiga. Alimsogelea tu na kusema kwa sauti ya chini, “Utamshukuru baba yako siku moja.”
Margaret alimtazama kwa macho yaliyokuwa yamejaa maumivu. “Au nitamlaumu kimya kimya maisha yangu yote.”
Kifo cha Mama Jonas
Majira ya baridi yalizidi. Kikohozi cha Bi. Eleanor kiligeuka kuwa kimya kibaya zaidi. Jonas alianza kutumia muda mwingi nyumbani, akimlisha supu, akimfunika blanketi, na kumwambia hadithi za uongo kuwa mambo yatakuwa sawa.
Usiku mmoja, mama yake alimuita karibu. Sauti yake ilikuwa nyembamba kama uzi uliokaribia kukatika.
Bi. Eleanor: “Jonas.”
Jonas: “Niko hapa, mama.”
Bi. Eleanor: “Yule binti... bado unampenda?”
Jonas: “Ndiyo.”
Bi. Eleanor: “Basi usimpende kwa kiburi. Mpende kwa uaminifu. Kama siku moja dunia itawapokonya kila kitu, hakikisha haikupokonya ukweli wenu.”
Jonas alimshika mkono. Ulikuwa mwepesi sana, kama mkono wa mtu aliyekuwa tayari ameanza kuondoka.
“Usiondoke,” Jonas alinong’ona.
Mama yake alitabasamu kwa uchovu. “Hakuna mtu anayebaki kwa sababu amependwa sana, mwanangu. Lakini upendo unaweza kubaki baada ya mtu kuondoka.”
Alifariki kabla alfajiri haijafika.
Siku ya mazishi, Margaret alifika kwa mbali akiwa na mama yake. Hakuweza kumsogelea Jonas mbele ya watu wote. Lakini wakati jeneza lilipokuwa likishushwa, Jonas aliinua macho na kumwona. Hakuwa amevaa mapambo. Hakuwa ametabasamu. Alikuwa pale tu, machozi yakimtoka kimya kimya.
Kwa Jonas, hilo lilitosha. Alijua hakubaki peke yake kabisa.
Uamuzi wa Margaret
Kifo cha mama Jonas kilibadilisha kitu ndani ya Margaret. Alitambua kuwa maisha hayangoji mtu amalize kuogopa. Hayangoji baba akubali. Hayangoji jamii ipate busara. Yalikuwa yanapita kama treni, na mtu akiendelea kusimama kituoni kwa hofu, siku moja angegundua safari zote zimeondoka.
Usiku mmoja, Margaret alimwambia mama yake ukweli.
“Sitamuoa Edward.”
Mama yake alikaa kimya.
“Nitamuoa Jonas, au sitaolewa kabisa.”
Mama yake alimtazama muda mrefu. Macho yake yalikuwa na hofu, lakini pia kulikuwa na kitu kingine. Kitu kama fahari iliyofichwa.
Mama yake: “Unajua baba yako hatakubali.”
Margaret: “Najua.”
Mama yake: “Unajua maisha na Jonas hayatakuwa rahisi.”
Margaret: “Maisha bila yeye ndiyo ambayo sitayaweza.”
Mama yake hakusema zaidi. Alisimama, akaenda kwenye kabati, akatoa kitambaa kidogo kilichofungwa. Ndani yake kulikuwa na sarafu chache na pete nyembamba ya zamani.
“Hii ilikuwa ya mama yangu,” alisema. “Sina ruhusa ya kukupa uamuzi, lakini ninaweza kukupa baraka ambazo sikuwahi kupewa mimi.”
Margaret alimkumbatia mama yake kwa muda mrefu. Kwa mara ya kwanza, alilia bila kujizuia.
Ndoa Ndogo
Jonas na Margaret walioana katika kanisa dogo lililokuwa pembezoni mwa mji, siku ya asubuhi yenye ukungu. Hakukuwa na sherehe kubwa. Hakukuwa na magari ya farasi yaliyopambwa. Hakukuwa na meza za chakula wala nyimbo nyingi.
Kulikuwa na mchungaji mzee, Mzee Samuel wa duka la vitabu, mama yake Margaret aliyekaa nyuma akifuta machozi, na watu wachache waliothubutu kuja bila kuogopa hasira ya Bwana Whitmore.
Baba yake Margaret hakuhudhuria.
Wakati Margaret alipotembea kuelekea mbele ya kanisa, Jonas alishindwa kuficha machozi. Alikuwa amepoteza mama yake, lakini siku hiyo alihisi kama maisha yamemrudishia sababu ya kuendelea.
Mchungaji: “Jonas, unamchukua Margaret kuwa mke wako?”
Jonas: “Ninamchukua, mbele ya Mungu, mbele ya dunia, na hata mbele ya wale wasiotuamini.”
Mchungaji: “Margaret, unamchukua Jonas kuwa mume wako?”
Margaret: “Ninamchukua. Siyo kwa sababu njia ni rahisi, bali kwa sababu moyo wangu umeichagua.”
Walipovalishwa pete, Margaret alihisi kana kwamba si pete tu imeingia kidoleni mwake. Ilikuwa ahadi. Ilikuwa vita. Ilikuwa safari.
Walitoka kanisani wakishikana mikono. Nje, treni ilipiga kingora kwa mbali. Margaret alitetemeka kidogo, lakini safari hii Jonas alikuwa karibu yake.
“Usiogope,” Jonas alisema.
Margaret alimtazama. “Niko na wewe.”
Hayo yalikuwa majibu yake yote.
Miaka Mitatu ya Furaha na Ukimya
Miaka ilipita. Jonas alifungua karakana ndogo ya useremala. Haikuwa kubwa, lakini ilikuwa yake. Alitengeneza milango, viti, masanduku na meza. Margaret alianza kuandika hadithi zake usiku baada ya kazi za nyumbani. Mara nyingine Jonas alimkuta amelala mezani, kalamu ikiwa bado mkononi.
Walikuwa maskini kwa vitu vingi, lakini walikuwa matajiri kwa namna walivyotazamana. Walicheka kwa vitu vidogo. Waligombana kwa mambo madogo zaidi. Jonas alisahau mara nyingi kuleta kuni. Margaret alikasirika akimkuta ameacha vipande vya mbao kila mahali. Lakini kila usiku walilala wakiwa wamesameheana.
Jambo moja tu lilibaki kama kivuli juu ya furaha yao.
Hawakupata mtoto.
Mwaka wa kwanza, watu waliwaambia wasubiri. Mwaka wa pili, watu walianza kuuliza. Mwaka wa tatu, watu walianza kunong’ona.
Margaret aliumia kimya kimya. Kila alipomwona mwanamke akimbeba mtoto wake sokoni, moyo wake ulijikunja. Alianza kujilaumu. Alianza kujiuliza kama baba yake alikuwa sahihi. Labda ndoa yake ilikuwa imebarikiwa na upendo lakini kunyimwa uzao.
Usiku mmoja, Jonas alimkuta akilia karibu na dirisha.
Jonas: “Margaret.”
Margaret: “Nimeshindwa kukupa mtoto.”
Jonas: “Hukuniahidi mtoto. Uliniahidi maisha.”
Margaret: “Lakini ungestahili kuwa baba.”
Jonas: “Na wewe ungestahili kuacha kujilaumu kwa jambo ambalo haliko mikononi mwako.”
Jonas alimkumbatia. Margaret alilia kifuani mwake mpaka machozi yakapungua. Usiku huo, walikaa muda mrefu bila kusema. Nje, treni ya usiku ilipita, kingora chake kikikatiza ukimya.
Margaret alishika mkono wa Jonas kwa nguvu.
“Kila nikisikia treni usiku,” alisema, “nahisi kama siku moja itatuita.”
Jonas akambusu kwenye paji la uso. “Ikituina, tutaenda pamoja.”
Barua Kutoka Mji Mwingine
Mwaka uliofuata, Jonas alipokea barua kutoka kwa mfanyabiashara mmoja wa mji wa mbali aliyekuwa amesikia kuhusu kazi zake za useremala. Alitaka Jonas ahamie huko kwa miezi kadhaa, labda mwaka mzima, ili asimamie karakana mpya na kutengeneza samani kwa nyumba kubwa zinazokuwa zikijengwa.
Malipo yalikuwa mazuri kuliko chochote walichowahi kupata. Yangeweza kuwapa nafasi ya kuanza upya mbali na minong’ono ya mji wao, mbali na macho ya baba yake Margaret, mbali na ukimya wa watu waliokuwa wakihesabu miaka yao ya ndoa bila mtoto.
Jonas alimwonyesha Margaret barua hiyo.
Alisoma kimya kimya.
Margaret: “Ni mbali.”
Jonas: “Ndiyo.”
Margaret: “Tutakwenda kwa treni?”
Jonas: “Ndiyo.”
Margaret alishika karatasi kwa muda mrefu. Uso wake ulionyesha hofu ileile ambayo Jonas alikuwa ameiona mara nyingi kila treni ilipopiga kingora karibu sana.
“Kama hutaki, hatuendi,” Jonas alisema.
Margaret alitikisa kichwa. “Hapana. Labda hii ndiyo nafasi yetu. Labda maisha yanataka tuondoke hapa.”
Jonas alimsogelea. “Basi tutaondoka pamoja.”
Margaret alitabasamu kwa uchungu. “Kama siku ile ndani ya treni?”
“Kama siku ile,” Jonas alisema. “Safari hii hakuna kibaka.”
Margaret hakujua kwa nini maneno hayo hayakumfariji kikamilifu.
Kabla ya Safari
Siku ya kuondoka ilipokaribia, Margaret alikwenda kumuaga mama yake. Baba yake hakutoka chumbani. Hakusema baraka wala laana. Ukimya wake ulikuwa ukuta wa mwisho kati yao.
Mama yake alimkumbatia muda mrefu.
Mama yake: “Umechagua maisha yako.”
Margaret: “Ndiyo.”
Mama yake: “Basi yaishi kwa moyo wote. Hata kama yatakuumiza, yaishi kama yako.”
Margaret alilia. Alijua huenda ilikuwa mara ya mwisho kumuona mama yake kwa muda mrefu. Hakujua kuwa ilikuwa mara ya mwisho kabisa.
Walipofika kituoni, treni ilikuwa tayari inafuka moshi. Jonas alikuwa na begi moja kubwa, Margaret alikuwa na sanduku dogo lenye nguo, barua zao, na maandishi machache aliyofanikiwa kuyaokoa.
Jonas alimsaidia kupanda. Margaret alisimama mlangoni kwa sekunde chache, akiangalia moshi, reli na injini kubwa iliyokuwa mbele.
Moyo wake ukapiga kwa nguvu.
“Margaret?” Jonas alimuita.
Aligeuka.
“Niko hapa,” alisema.
Jonas akamshika mkono. “Najua.”
Waliingia ndani na kukaa karibu na dirisha. Treni ilianza kusogea taratibu. Mji wao ukaanza kubaki nyuma. Margaret alitazama nje mpaka nyumba za mwisho zilipopotea.
Jonas alimshika mkono chini ya siti. Margaret aliuacha mkono wake ndani ya mkono wa Mumewe.
Kwa muda, kila kitu kilionekana kuwa salama.
Kisha upepo ukabadilika.
Ajali
Treni ilikuwa imepita zaidi ya saa moja njiani wakati mvua ilipoanza. Mwanzoni ilikuwa nyepesi. Matone madogo yaligonga madirisha kwa sauti ya upole. Baadaye upepo ukawa mkali, anga likawa jeusi, na treni ikaanza kutikisika zaidi kuliko kawaida.
Margaret alishika mkono wa Jonas kwa nguvu.
“Kuna kitu hakiko sawa,” alisema.
Jonas alimtazama nje. Reli ilikuwa ikipinda kuelekea eneo la bonde. Injini ilipiga kingora mara moja. Kisha mara ya pili. Mara ya tatu ilisikika kama kelele ya kuomba msaada.
Watu ndani ya behewa walianza kutazamana. Mtoto alilia. Mwanamke mmoja akaanza kusali. Mwanaume mmoja akasimama, lakini treni ilitikisika ghafla akagonga upande wa siti.
Halafu sauti ya chuma ilipasua hewa.
Ilikuwa sauti ambayo Margaret angeitambua hata katika maisha mengine.
Breki zililia kwa maumivu. Behewa likayumba. Watu wakapiga kelele. Sanduku likaanguka kutoka juu, dirisha likapasuka, moshi ukaingia ndani. Jonas alimvuta Margaret karibu yake, akijaribu kumkinga.
Margaret: “Jonas!”
Jonas: “Shika mkono wangu!”
Margaret: “Ninaogopa!”
Jonas: “Niko hapa!”
Treni iliruka kutoka kwenye reli.
Kila kitu kilitokea kwa sekunde chache, lakini kwa Margaret zilionekana kama miaka. Aliona mwanga. Akasikia mbao zikivunjika. Akasikia kelele za watu. Akasikia jina lake likiitwa.
Behewa lilipinduka.
Kisha giza.
Alipofungua macho, hakujua alikuwa wapi. Kila sehemu ilijaa moshi, mvua na harufu ya makaa ya mawe. Alikuwa amelala pembeni ya kiti kilichovunjika. Kifua chake kilikuwa kinauma. Alijaribu kusogea, lakini mwili wake haukumtii.
“Jonas...” alinong’ona.
Kwa mbali, alisikia kikohozi. Kisha sauti yake.
“Margaret.”
Aligeuza kichwa kwa shida. Jonas alikuwa karibu naye, damu ikitoka upande wa uso wake. Mkono wake ulikuwa umenyooshwa kuelekea kwake, lakini haukumfikia.
Margaret alijitahidi kusogea. Maumivu yakamkata pumzi. Jonas naye alijivuta kwa nguvu zake za mwisho. Hatimaye vidole vyao vikagusana.
Nje, mvua iliendelea kunyesha. Watu walipiga kelele kwa mbali. Moto mdogo ulikuwa umeanza sehemu ya mbele ya treni. Lakini kwao, dunia ilikuwa imebaki kwenye nafasi ndogo kati ya mikono yao miwili.
Jonas: “Usiogope.”
Margaret: “Ulisema treni haitachukua chochote.”
Jonas: “Basi ikituchukua... nitakutafuta tena.”
Margaret: “Usiniache.”
Jonas: “Kama kweli roho haifi, nitakutafuta. Hata kama itachukua miaka mia moja.”
Margaret: “Na mimi nitakusubiri.”
Jonas alijaribu kubana mkono wake, lakini nguvu zake zilikuwa zinapungua. Margaret alimtazama kupitia machozi. Hakusikia tena kelele za watu. Hakusikia mvua. Hakusikia moto. Alisikia tu pumzi ya Jonas ikipungua taratibu.
“Margaret,” Jonas alinong’ona kwa mara ya mwisho.
“Niko hapa,” alisema.
Maneno hayo yalikuwa ya mwisho kutoka kinywani mwake.
Mikono yao ilibaki imeshikana.
Waliwakuta hivyo alfajiri iliyofuata.
Miili Miwili, Ahadi Moja
Walizikwa pamoja kwenye eneo dogo karibu na kanisa la mji wa mbali ambao hawakuwahi kuufikia wakiwa hai. Hakukuwa na familia nyingi. Hakukuwa na sherehe. Hakukuwa na hadithi ndefu kuhusu mapenzi yao.
Mzee Samuel alisafiri siku mbili kufika kwenye mazishi. Alisimama karibu na makaburi yao, akiwa ameshika kitabu cha zamani ambacho kilikuwa kimebeba barua zao za mwanzo.
Mama yake Margaret hakufika. Habari zilimfikia akiwa mgonjwa kwa maumivu ambayo hakuna daktari angeweza kuyapima. Baba yake alipokea taarifa hiyo akiwa amekaa sebuleni. Kwa mara ya kwanza, gazeti lilidondoka mikononi mwake.
Hakusema kitu.
Lakini usiku huo, watu wa nyumba yao walisikia mwanaume mzito akilia peke yake.
Mvua ilinyesha juu ya makaburi ya Jonas na Margaret kwa siku tatu. Baadaye jua likachomoza. Mji ukaendelea. Treni nyingine zikapita. Watu wengine wakasafiri. Dunia ikafanya kile inachofanya vizuri zaidi: kuendelea mbele hata baada ya mioyo fulani kusimama.
Lakini mahali pasipoonekana, ahadi yao haikufa.
Ilibaki ikining’inia kwenye reli, kwenye moshi, kwenye harufu ya makaa ya mawe, na kwenye kingora cha treni kilichokuwa kikilia kila usiku kama kinaita majina mawili yaliyopotea.
Miaka ikapita.
Karne zikapita.
Majina yakasahaulika.
Miji ikabadilika.
Treni za mvuke zikawa historia.
Lakini ahadi yao iliendelea kusafiri.
Mpaka siku moja, zaidi ya miaka mia mbili baadaye, kingora kingine kilipiga mbali sana kutoka Ohio.
Safari hii hakikuwa kingora cha treni ya mvuke.
Kilikuwa kingora cha SGR.
Dar es Salaam.
Mwaka 2025.