TULIKUTANA TENA-SURA YA 4
Kingora cha SGR
TULIKUTANA TENA: Mapenzi Yaliyoshinda Karne
Mwaka 2025, Dar es Salaam ilikuwa imeamka kwa haraka yake ya kawaida. Magari yalikuwa yakisukumana barabarani, bodaboda zilikuwa zikichana nafasi nyembamba kati ya foleni, na watu walikuwa wakitembea kwa kasi ya mtu anayehisi maisha yanamkimbia nyuma.
Kituo cha SGR kilikuwa kimejaa wasafiri. Mabegi yaliburutwa sakafuni. Watoto walishika mikono ya wazazi wao. Watu waliokuwa wamechelewa walikuwa wanakimbia huku wakitazama tiketi zao kwenye simu. Kila kitu kilikuwa cha kisasa, safi na chenye mpangilio.
Lakini kwa Maya, kila kitu kilikuwa kimepoteza mpangilio wake.
Alisimama mbele ya behewa la tatu, mikono yake ikiwa imekaza kwenye mkoba wake. Alikuwa na miaka ishirini na sita. Alikuwa amevaa gauni jepesi la rangi ya bluu iliyopauka, nywele zake zikiwa zimefungwa nyuma kwa haraka. Kwa macho ya mtu mwingine, angeonekana kama msafiri wa kawaida anayesubiri kuingia ndani.
Lakini ndani yake, kulikuwa na vita.
Kingora cha treni kilipopiga, kifua chake kilikaza. Sauti hiyo ilipasua akili yake kama kisu kilichogusa jeraha la zamani. Kwa sekunde moja, kituo cha Dar es Salaam kilitoweka mbele ya macho yake. Akaona moshi mweusi. Akaona mvua. Akaona dirisha la mbao likipasuka. Akaona mkono wa mwanaume ukimtafuta gizani.
Akarudi kwenye hali ya kawaida kwa mshtuko.
Mhudumu: “Dada, tafadhali panda. Muda umefika.”
Maya: “Na... naweza kusubiri kidogo?”
Mhudumu: “Milango inafungwa muda si mrefu.”
Maya alitaka kusogea. Miguu yake haikutii. Hakuwa mtu wa kuogopa safari. Alikuwa amepanda mabasi, ndege na magari ya kila aina. Lakini treni zilikuwa tofauti. Tangu akiwa mdogo, kila aliposikia kingora cha treni, moyo wake ulipiga kwa hofu ambayo hakuweza kuieleza.
Mama yake aliwahi kumwambia ni mawazo tu. Rafiki zake walimtania kuwa alikuwa anaangalia filamu nyingi. Mpenzi wake, Kelvin, alimwambia mara nyingi kuwa alipaswa kuwa mtu mzima na kuacha kuogopa vitu vya kawaida.
Lakini hofu hiyo haikuwa ya kawaida.
Haikuwa inatoka kwenye akili.
Ilikuwa inatoka mbali zaidi.
Kijana Aliyekuwa Amechelewa
Wakati Maya akiwa bado amesimama, kijana mmoja alikuwa akikimbia kutoka upande wa lango la kuingilia. Alikuwa amebeba begi dogo begani, shati lake la bluu likiwa limetoka upande mmoja, na uso wake ukiwa umejaa jasho la mtu aliyekuwa amechelewa kwa sababu ambazo dunia haikujali.
Jina lake lilikuwa Jaden.
Alikuwa amekosa usingizi usiku uliopita. Siyo kwa sababu ya safari tu, bali kwa sababu maisha yake yalikuwa yamejaa maamuzi ambayo hakuwa ameyamaliza. Alikuwa anaenda Dodoma kwa kazi ya siku mbili, lakini nyuma yake Dar es Salaam kulikuwa na mchumba wake, Irene, ambaye alikuwa amechoka na tabia yake ya kuwa mbali hata akiwa karibu.
“Jaden, wewe upo na mimi au upo na mawazo yako?” Irene alikuwa amemuuliza usiku uliopita.
Hakujua ajibu nini.
Alimpenda Irene kwa namna ya heshima. Alimzoea. Walikuwa wamepanga maisha pamoja kwa sababu kila mtu karibu yao alisema walifaa. Lakini ndani yake, kulikuwa na nafasi tupu ambayo Irene hakuijaza. Na Jaden alichukia ukweli huo.
Alipokimbia kuelekea behewa la tatu, macho yake yakatua kwa Maya.
Alisimama kwa nusu sekunde.
Hakumjua.
Lakini moyo wake ulifanya kitu cha ajabu. Ulipiga kwa nguvu, si kwa mshangao wa kawaida, bali kama mtu aliyesikia jina lake likiitwa na mtu aliyekuwa amekufa zamani.
Mlango wa treni ukaanza kutoa sauti ya tahadhari.
Jaden alifika karibu yake.
Jaden: “Dada, unaingia au unaaga treni?”
Maya: “Siwezi...”
Jaden: “Unaweza. Hata kama miguu yako haijakubali bado.”
Maya alimgeukia. Macho yao yalipokutana, hofu yake haikuisha mara moja, lakini ilibadilika. Ikawa kitu kingine. Kama mwili wake ulikuwa umemkumbuka mtu kabla ya akili yake kufanya hivyo.
Mlango ukaendelea kufungwa.
Jaden hakutaka kufikiria sana. Alimshika mkono.
Maya hakupinga.
Waliingia ndani sekunde chache kabla mlango haujafungwa kabisa.
Treni ikaanza kusogea.
Siti Moja, Safari Moja
Ndani ya behewa, Maya alisimama kwa sekunde kadhaa akijaribu kutuliza pumzi. Jaden alimuachia mkono polepole, kana kwamba naye alikuwa amegundua wamekaa muda mrefu zaidi ya ulivyohitajika.
Jaden: “Samahani kama nimekuvuta kwa nguvu.”
Maya: “Umeniokoa au umeniteka?”
Jaden: “Inategemea ukifika Dodoma utakuwa bado unanilaumu au utanipa asante.”
Maya alijikuta akicheka. Kicheko hicho kilimtoka bila ruhusa. Kilikuwa kicheko kidogo, lakini kilitosha kuvunja kamba ya hofu iliyokuwa imemkaza shingoni.
Walitafuta viti vyao. Jaden alitoa tiketi yake kwenye simu, Maya akatoa yake. Walipotazama namba za siti, wote wawili wakanyamaza.
Walikuwa siti moja.
Dirisha moja.
Safari moja.
Jaden alimtazama Maya, akainua nyusi kidogo.
Jaden: “Hii sasa ni hatari. Kama unanichukia, una masaa kadhaa ya mateso mbele yako.”
Maya: “Na kama sikuchukii?”
Jaden: “Basi treni imefanya kazi nzuri kuliko apps za dating.”
Maya alicheka tena. Safari hii kwa uhuru zaidi.
Walikaa. Maya upande wa dirisha, Jaden pembeni yake. Treni ilianza kuongeza mwendo. Majengo ya Dar es Salaam yakaanza kurudi nyuma. Watu ndani ya behewa wakatulia, wengine wakitoa simu, wengine wakifungua vitafunwa, wengine wakianza usingizi mapema kama walikuwa wamepanda treni kwa ajili ya kulipiza kisasi kwa usiku uliopita.
Maya alitazama nje. Kwa sekunde chache alihisi harufu ya makaa ya mawe.
Aligeuka haraka.
“Umesikia harufu yoyote?” aliuliza.
Jaden alimwangalia. “Harufu gani?”
“Kama... moshi. Makaa.”
Jaden alikaa kimya kwa muda. Kisha akatabasamu kidogo, lakini macho yake yalionyesha alikuwa ameguswa na kitu.
“SGR haina makaa,” alisema.
“Najua.”
“Basi labda una kumbukumbu za treni za zamani.”
Maya aligeuka kumwangalia. “Umesema nini?”
Jaden akacheka ili kupunguza uzito wa maneno yake. “Nimetania tu.”
Lakini ndani yake, hakutania kabisa.
Advertisement
Mazungumzo Yaliyokuja Kirahisi
Safari ilipoendelea, mazungumzo yao yalipanuka bila kupanga. Maya alijua jina lake ni Jaden, alikuwa mbunifu wa mifumo ya kidigitali na alikuwa anaenda Dodoma kwa kikao cha kazi. Jaden alijua Maya alikuwa mtaalamu wa mawasiliano, alikuwa anaenda Dodoma kumtembelea dada yake na pia kukimbia kidogo kelele za Dar es Salaam.
“Kukimbia?” Jaden aliuliza.
Maya alitazama nje kwa muda. “Wakati mwingine mtu hakimbii sehemu. Anakimbia maswali.”
“Na Dodoma ina majibu?”
“Sijui. Lakini angalau haina watu wengi wanaoniuliza kwa nini sijaolewa bado.”
Jaden alicheka. “Hilo swali linakufuata mpaka kwenye treni.”
Maya akamwangalia. “Na wewe?”
“Na mimi nini?”
“Una mtu anayekuuliza lini utaoa?”
Jaden alichelewa kujibu. Huo ucheleweshaji mdogo ulisema zaidi kuliko jibu lake.
“Nina mtu,” alisema hatimaye.
Maya aligeuza uso kidogo. “Mpenzi?”
“Ndiyo.”
“Unampenda?”
Jaden alicheka kwa wasiwasi. “Hilo ni swali la saa ngapi kwenye safari?”
“La kabla hatujafika Morogoro.”
Jaden alitazama mikono yake. “Namheshimu sana.”
Maya hakusema kitu.
Jaden alimwangalia. “Hilo halikutosha, si ndiyo?”
“Sijasema.”
“Lakini umefikiria.”
“Mimi pia nina mtu,” Maya alisema taratibu.
Jaden alitabasamu kwa namna ambayo haikuwa furaha. “Unampenda?”
Maya alitazama nje. Nje, miti ilikimbia nyuma ya dirisha.
“Ananipenda,” alisema.
Jaden alielewa. Wote wawili wakakaa kimya kwa muda. Lakini kimya hicho hakikuwa cha wageni. Kilikuwa cha watu wawili waliogundua kuwa wameleta mizigo ndani ya safari ambayo haikuwa imewaomba mizigo hiyo.
Kelvin na Irene
Simu ya Maya iliita. Jina la Kelvin likaonekana kwenye screen. Alisita kabla ya kupokea.
Kelvin: “Umeingia kwenye treni?”
Maya: “Ndiyo.”
Kelvin: “Umeona? Hakukuwa na sababu ya kuogopa. Unapenda sana drama.”
Maya: “Kelvin...”
Kelvin: “Nikifika jioni nitakupigia. Usisahau tumepanga kuongea kuhusu tarehe ya kupeleka posa.”
Maya hakujibu mara moja. Jaden alijifanya anaangalia nje, lakini hakuhitaji kusikiliza sana kujua mazungumzo hayo hayakuwa mepesi.
Maya alipokata simu, alifunga macho kwa sekunde chache.
“Yeye ndiye huyo?” Jaden aliuliza kwa sauti ya chini.
“Ndiyo.”
“Anakujua?”
“Anafikiri ananijua.”
Simu ya Jaden nayo iliita muda mfupi baadaye. Irene.
Alipokea.
Irene: “Umeingia?”
Jaden: “Ndiyo.”
Irene: “Usisahau kuongea na kaka yangu ukifika. Ile kazi ya ofisini kwake inaweza kukusaidia sana.”
Jaden: “Nitajitahidi.”
Irene: “Jaden, usijitahidi. Fanya. Huwezi kuendelea kuishi kwa miradi midogo midogo milele.”
Alikata simu akiwa kimya. Maya alimwangalia, lakini hakumuuliza. Wakati mwingine mtu mgeni anaweza kukuheshimu zaidi kuliko mtu anayesema anakupenda.
Jaden aliweka simu pembeni.
“Sasa tumebaki wawili wenye watu wanaotupenda kwa namna inayotuumiza,” alisema.
Maya alicheka kwa huzuni. “Inaonekana treni hii imebeba mizigo mingi kuliko mabegi.”
Ndoto ya Mvua na Moshi
Baada ya muda, Maya alichoka. Usingizi ulimchukua taratibu, kichwa chake kikiegemea dirishani. Jaden alikaa kimya, akimtazama kwa muda mfupi kabla hajaamua kuangalia nje ili asionekane anamwangalia sana.
Maya alipoingia usingizini, ndoto ilimvamia bila huruma.
Alikuwa ndani ya treni nyingine. Si hii. Kulikuwa na mbao, moshi, mvua na kelele za watu. Alivaa gauni refu la zamani. Mikono yake ilikuwa na damu. Mwanaume fulani alikuwa karibu naye, akimtafuta gizani.
“Margaret!”
Alitaka kujibu, lakini koo lake lilikuwa limekauka.
“Shika mkono wangu!”
Treni ilitikisika. Dirisha likapasuka. Mvua ikaingia. Akahisi vidole vya mtu vikigusa vyake. Akajitahidi kuvishika.
“Usiniache,” alisema ndani ya ndoto.
“Nitakutafuta tena.”
Maya alishtuka kwa nguvu.
Alikuwa ameshika mkono wa Jaden.
Wote wawili walitazamana.
Kwa sekunde chache hakuna aliyesema kitu. Maya aliachia mkono wake haraka, uso wake ukijaa aibu.
Maya: “Samahani. Nilikuwa nimeota.”
Jaden: “Ndoto mbaya?”
Maya: “Sijui. Ilikuwa kama kumbukumbu.”
Jaden hakujibu. Kwa sababu neno hilo lilimgusa.
Kumbukumbu.
Tangu utoto, alikuwa na ndoto zinazojirudia. Treni ya zamani. Mwanamke anayelia. Mkono unaomtafuta. Kila alipoamka, alikuwa akisikia jina lisilo lake likizunguka kichwani.
Jonas.
Hakuwahi kumwambia mtu. Hata Irene. Hata mama yake.
Alimtazama Maya kwa muda mrefu kidogo.
“Uliota nini?” aliuliza.
Maya alitikisa kichwa. “Ukisema kwa sauti, ndoto nyingine zinakuwa halisi sana.”
Jaden alielewa, hata kama hakupaswa kuelewa.
Dodoma Inakaribia
Kadiri treni ilivyokaribia Dodoma, mazungumzo yao yalikuwa yamebadilika. Hayakuwa tena ya utani tu. Kulikuwa na tahadhari. Kulikuwa na mvuto. Kulikuwa na hofu kwamba wakisema sana, watafungua mlango ambao hawatajua kuufunga.
Maya alitazama saa. “Tunakaribia.”
Jaden akatikisa kichwa. “Ndiyo.”
“Baada ya hapa kila mtu anarudi kwenye maisha yake.”
“Maisha yake au watu wake?”
Maya hakujibu.
Treni ilipunguza mwendo. Sauti ya matangazo ikasikika ikitaja kituo cha Dodoma. Wasafiri wakaanza kujiandaa kushuka. Maya alishika mkoba wake. Jaden akachukua begi lake.
Waliposimama kwenye njia ya kutoka, ukaribu wao ulirudi. Watu walikuwa wamesongamana, lakini kwao dunia ilikuwa imepungua mpaka kuwa nafasi ndogo kati yao.
Jaden: “Naweza kukuomba kitu?”
Maya: “Kama si mkono wangu tena.”
Jaden: “Namba yako.”
Maya alitazama pembeni. Alijua hakupaswa. Kelvin alikuwa kwenye maisha yake. Jaden alikuwa na Irene. Walikuwa wamekutana ndani ya treni kwa bahati. Bahati nyingine zinapaswa kuachwa pale zinapotokea.
Lakini moyo wake haukukubali.
Alimpa namba.
Jaden aliiandika, kisha akamtumia ujumbe mfupi ili awe na yake.
Milango ilipofunguka Dodoma, joto la mji liliwapokea. Watu wakaanza kutoka. Maya na Jaden walitembea pamoja kwa hatua chache, kisha wakasimama.
Hakuna aliyejua namna ya kuagana.
Hatimaye Maya alisema, “Asante kwa kunisaidia kuingia.”
Jaden akamwangalia. “Nahisi si mara ya kwanza.”
Maya aliganda.
“Unamaanisha nini?”
Jaden alionekana kujuta mara moja. “Sijui. Nimesema tu.”
Walisimama kimya kwa sekunde chache. Kisha Maya akageuka na kuondoka. Baada ya hatua kadhaa, aligeuka tena. Jaden bado alikuwa pale, akimtazama.
Simu yake ikaita.
Kelvin.
Jaden naye alitazama simu yake.
Irene.
Wote wawili hawakupokea mara moja.
Na hapo, katikati ya kituo cha Dodoma, safari ambayo ilidhaniwa imeisha ilikuwa ndiyo kwanza imeanza.